Rasmi: Okwi Aachana na Simba, Atimkia Uarabuni

NYOTA wa Simba, Emmanuel Okwi, amejiunga na timu ya Fujairah Footbal Club inayoshiriki Ligi Kuu ya Falme za Kiarabu (UAE), imeelezwa.

 

Okwi ambaye msimu wa 2018/19 akiwa ndani ya Simba alifunga jumla ya mabao 15 na anashikilia rekodi ya kufunga ‘hat trick’ nyingi kuliko wote akifunga jumla ya mbili, ameshindwa kuelewana na mabosi zake Simba.

 

Chanzo cha habari kutoka nchini Uganda, kimeelezwa kuwa miongoni mwa timu ambazo zilikuwa zinahitaji huduma yake ni pamoja na Simba ambao walishindwana naye kwa dau alilohitaji kuwekewa mezani huku klabu nyingine ambazo ni pamoja na Kaizer Chief ya Afrika Kusini ilitajwa kuwa miongoni mwa timu iliyokuwa inahitaji saini yake.

 

“Wamekubaliana, nafikiri hatarudi Simba. Inaonekana msimu huu alitaka kuondoka na kujaribu sehemu nyingine, ndiyo maana aliwaambia wasubiri,” kilieleza.

 

Okwi alifanikiwa kuiongoza vyema timu ya taifa ya Uganda (The Cranes) hadi kucheza hatua ya 16 Bora ya Afcon nchini Misri, yeye akifunga mabao mawili.

 

Juhudi kubwa za Simba kumbakiza zimeonekana kukwama baada ya Mganda huyo kufanikiwa kutega mitego yake vizuri akiwasisitiza Simba kwamba atazungumza nao baada ya michuano ya Afcon.

 

Hata hivyo, baada ya kufanya vyema katika Afcon, huku akiwa mchezaji huru, Okwi akawa na nafasi kubwa zaidi ya kusajiliwa na timu nyingine akiingiza fedha nyingi zaidi kuliko angebaki Simba.

 

mganda huyo amekuwa bora uwanjani lakini mwenye akili nyingine ya kujua afanye nini inapofikia wakati wa usajili. Mara ya kwanza aliondoka Simba akiuzwa nchini Tunisia, baadaye alirejea tena na kuuzwa nchini Denmark lakini sasa ameondoka akiwa huru.

 

Fujairah FC ilianzishwa mwaka 1968 na imewahi kunyakua Kombe la Ligi Kuu ya UAE mara tatu, msimu wa 1985–86, 1989–90 na 2005–06. Msimu uliopita ilimaliza ikiwa nafasi ya 12 kati ya timu 14.

HISTORIA YA OPERATION ENTEBBE (Part 1)

HISTORIA YA OPERATION ENTEBBE (Part 1)

Loading...

Toa comment