The House of Favourite Newspapers

RUBY AFUNGUKIA KUBUMA, KUACHA MUZIKI !

Hellen George ‘Ruby’

TAJA wanamuziki wa kike wakali Bongo. Si jambo geni kwa mpenzi wa muziki mtaani kumuuliza mwenzake na si ajabu kusikia aliyeulizwa akimtaja mwanadada Hellen George ‘Ruby’. Ruby ni mwanamuziki ambaye, mbali na kufanya vizuri ndani ya Bongo, amefanikiwa kuupeleka muziki wake hata nje pia.

Kwa wanaokumbuka mwaka 2016, aliungana na mwanamuziki mkali Afrika, Yemi Alade kwenye msimu wa nne wa shoo za Coke Studio na kutengeneza wimbo mkali, ambapo wimbo wake wa Forever, ndiyo ulitumika kwenye kolabo hiyo. Kwa namna moja au nyingine kolabo hii ilimuongezea mashabiki na kumsogeza mbele kidogo kwenye tasnia ya muziki Afrika.

Lakini kuonyesha kwamba mwanadada huyu anaufahamu muziki vilivyo, amefanya ‘cover’ ya ngoma nyingi, baadhi yake ni wimbo wa Aslay uitwao Baby, Wimbo wa Je Utanipenda wa Diamond Platnumz na Sitabaki Kama Nilivyo wa Joel Lwaga.

Wazungu wanasema yupo ‘flexible’, Waswahili tunasema ‘anaweza’, Wasambaa wanasema ‘aadaha’, Wahaya wanasema ‘nnabasa’ na Wachaga wanasema ‘akeidima!’ Huyo ndiyo Ruby. Hata hivyo pamoja na ukali wake, lakini kuna muda amekuwa akisuasua. Mwendo wa kufika mbali zaidi kimuziki unaonekana ni wa kobe tofauti na watu walivyokuwa wanamtarajia. Nini shida?

Watu wengi wanaweza kujiuliza swali hili. Majibu wanayoweza kuyapata yanaweza kuwa tetesi wanazozisikia.

Mara anatumia dawa za kulevya. Mara hivi mara vile. Kuhusu matumizi ya dawa za kulevya amekwisha zungumzia hilo. Kwamba hatumii. Lakini vipi kuhusu mambo mengine anasema nini? Ungana naye kwenye mahojiano haya na Amani.

Amani: Soko la muziki limebadilika Ruby, tunaona wanamuziki wengi kwa sasa wakitoa kazi mpya wanasindikiza na video, imekuwaje umeamua kutoa Wimbo wa Ntade bila video?

RUBY: Unajua nilikaa muda mrefu bila kufanya kazi. Nimejaribu kufanya ‘bonus truck’ ili kuona mwamko wa mashabiki ambao ndiyo utanihamasisha zaidi kufanya kazi.

Amani: Kusipokuwa na mwamko mkubwa muziki ndiyo utapiga chini?

RUBY: Hapana. Lakini tayari mwamko nimeshaona ni mkubwa. Ninashukuru kwa mahojiano haya na kuwafahamisha mashabiki zangu.

Amani: Hivi karibuni mwanamuziki kutoka Nigeria, Davido alikuja Bongo na ukapata nafasi ya kuwa naye karibu pamoja na kufanya naye shoo, kuna lolote pengine tutegemee kutoka kwenu?

RUBY: Siwezi kujibu hili, lipo ndani ya uongozi wangu. Wao wana nafasi ya kulizungumzia zaidi.

Amani: Watu wanakutegemea kimataifa zaidi, lakini mbio zako zinaonekana ni za kobe, nini tatizo?

RUBY: Tatizo sipati sapoti ninayostahili ya kunipeleka kimataifa.

Amani: Unamaanisha sapoti kutoka kwa mashabiki au wapi?

RUBY: Ndiyo. Kwa mashabiki na hata kwenye media. Nisapotini zaidi nitafika huko.

Amani: Kwa upande wako ukipata sapoti ni mwanamuziki gani wa nje utaanza naye kazi?

RUBY: Sijatageti mwanamuziki mmoja. Wengi tu nitafanya nao kazi.

Amani: Mwanamuziki gani wa kike unamzimia Bongo?

RUBY: Sipendi wanamuziki wa kike. Mimi ni mshabiki wa wanamuziki wa kiume.

Amani: Huyo wa kiume unayemzimia ni nani?

RUBY: Ni wengi sina mmoja wa kumtaja.

Amani: Upo kwenye uhusiano wa kimapenzi?

RUBY: Mashabiki wangu hawana haja ya kufahamu juu ya hilo, wakifahamu kuhusu kazi zangu inatosha.

Amani: Haja wanayo, kwa sababu ni mashabiki zako wanatakiwa kufahamu pia ‘life style’ yako na watu wanaokuzunguka?

RUBY: Hapana. Sipo tayari kumuweka wazi.

Amani: Nje ya muziki unajishughulisha na nini zaidi?

RUBY: Hakuna. Lakini huko mbeleni yakitokea mambo ambayo nitakuwa tayari kuyazungumza ‘public’ nitayazungumza na wala hakuna shida.

Amani: Asante kwa ‘time’ yako Ruby.

RUBY: Shukurani kwa nafasi na sapoti pia.

Makala: Boniphace Ngumije

Comments are closed.