The House of Favourite Newspapers

RUGE, MENGI WALIVYOKUTANA NA SOMO LA MAISHA YAO DUNIANI!

NI usiku mnene, nipo kwenye mkutano ambao sijui unahusiana na nini. Licha ya kuwa na mwanga hafifu katika ukumbi, nawaona watu wengi waliomo ndani wamepiga makoti meusi tupu na mashati meupe.

 

Hakuna aliyekuwa anaongea, kila mmoja yupo bize kwenye laptop yake. Wakati nikiwa nawaza nipo kwenye mkutano gani na waliomo humo ni kina nani, nikaona watu wawili wameongozana kutoka katika lango kuu.

Nilipowatazama kwa makini nikagundua ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba akiwa anaonekana kumuelekeza jambo Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi. Akili yangu ikawa kwenye hofu maana nawajua wawili hao wote wametangulia mbele za haki kwa nyakati tofauti.

 

Baaada ya Ruge kumuonesha sehemu ya kukaa na mimi nikawafuata karibu yao na kusikiliza mazungumzo yao. Mambo yalikuwa hivi;

Ruge: Karibu mwalimu wangu, vipi huko duniani wanaendeleaje?

Mengi: Sikutimiza ndoto zangu za kusaidia watu. Bado nilikuwa na ndoto za kugusa maisha ya watu hususan maskini.

Ruge: Hilo hata mimi kwa kweli nimelifanya, hakika Watanzania watakuwa wanatukumbuka kwa hilo. Nilijitahidi kufundisha namna ya kuchangamkia fursa kwa vijana.

 

Mengi: Sina hakika kama watatukumbuka, lakini kwa kweli nimekuwa nikijitahidi sana kufanya kila ninaloweza kuhakikisha ninasaidia wahitaji…

Ruge: Najua sasa hivi mzee walemavu watakuwa wanakulilia, Serengeti Boys ndiyo kabisa, tasnia ya habari ndiyo usiseme, familia yako ndiyo pigo kubwa zaidi kwao!

Mengi: Hata wewe kijana ulinipa fundisho kubwa sana, sikutegemea kama msiba wako ungekuwa mkubwa kiasi kile, uniwie radhi kwa fikra hizo nilizokuwa nazo.

 

Ruge: Hahaha usijali mzee wangu, kikubwa ni kujitahidi tu mtu unapokuiwa duniani kuacha alama, kuna ambao wanaacha alama za ujambazi, ulevi, uzinzi na mambo mengine yasiyofaa.

Mengi: Kabisa…japo desturi za Watanzania si kuwasema vibaya marehemu lakini inapotokea wanakuzungumza kwa mazuri ni jambo jema sana.

Ruge: Ila Wabongo mzee wangu siyo wa kuwaamini sana, unaweza kukuta hata wewe wapo wanaokusema vibaya…

 

Mengi: Najua, hilo ni lazima huwezi kuwazuia watu wasizungumze, lakini kikubwa ni kila mmoja kujitafakari safari yake. Unaweza kuwa unamsema mwenzako ana dhambi kumbe wewe ndiyo ukawa na dhambi zaidi, hakuna sababu ya kunyoonesheana vidole.

Ruge: Kitu gani ambacho ulitamani kukiona pengine kule duniani kabla hujaja huku?

Mengi: Aisee vingi sana, nilitamani kuona kiwanda changu cha magari nilichokuwa nataka kukianzisha, nilitamani kuona kiwanda cha simu za kisasa…

 

Ruge: Kwa kweli ulikuwa na ndoto kubwa, mimi maisha yangu nilitamani kufundisha zaidi mbinu za ujasirimali hususan kwa vijana, hilo ndilo deni kubwa ninaloliona nilikuwa bado nahitajika kulifanya.

Mengi: Nilikuwa naona, hakika mbegu uliyopanda kwenye mioyo ya watu haitasahaulika, ni fundisho pia kwa wengi tuliowaacha kule.

Ruge: Hivi vijana wameshailelewa dhana ya ujasiriamali au bado wanaishi kwa kuamini ndoto za kuajiriwa?

Mengi: Kwa kiasi kikubwa nimeona somo kama limeshawaka, wengi hawaamini katika ajira zaidi ya kujiajiri wao wenyewe katika biashara mbalimbali.

 

Ruge: Ni jambo jema, sema nini, Rais Dk John Pombe Magufuli ana maono ya mbali, naamini ipo siku Watanzania watakuja kumuelewa, yule bwana anataka matokeo na siyo maneno. Anataka maendeleo na siyo siasa, hataki kuishi kwa ujanjaujanja…

Mengi: Ujanjaujanja sasa hivi umeisha, usipokuwa na shughuli Dar mwenyewe utarudi kijijini. Watu wamejifunza nidhamu ya fedha, hawatumii hovyohovyo kama ilivyokuwa zamani.

 

Ruge: Hilo nilikuwa nawaambia wasanii wengi niliokuwa nafanya nao kazi, nafikiri kwa sasa watakuwa wamenielewa…vipi rafiki yangu Sugu (Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya-Mjini) yupo? Anaendeleaje?

Mengi: Sugu juzijuzi alipata ugeni wa Rais Dk John Pombe Magufuli, alinifurahisha sana kijana kwa kusema anamuunga mkono rais akiwa chama pinzani. Kwangu mimi naona ni ukomavu wa kisiasa, kuwa mpinzani siyo kupinga kila kitu na hilo ndilo wengi hukosea.

Wakiwa kwenye mazungumzo hayo, ghafla nikawaona wamenitolea macho kama ambao wanataka kuniuliza jambo. Mimi nikawa nimewatolea macho tu, mara nikashtuka. Kumbe nilikuwa naota bwana, mazungumzo hayo yalijia ndotoni na si uhalisia.

Comments are closed.