MFANYABIASHARA James Rugemarila ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Januari 24, 2020, alikutana na mwakilishi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) alipokuwa ametembelea gerezani na kumkabidhi nakala ya barua aliyoiandika kwenda kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) jinsi benki ya Standard Chartered Hong Kong walivyokwepa kodi.
Hiyo imekuja baada ya Wakili wa Takukuru, Maghela Ndimbo, kuiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi katika shauri hilo haujakamilika.
Rugemarila amesema kuwa ndani ya barua hiyo ameeleza ni jinsi gani benki ya Standard Chartered Hong Kong walivyokuwa wakikwepa kodi ya ushuru wa forodha kwa hiyo hadi sasa hajapata mrejesho hivyo akaiomba mahakama kesi itakapotajwa tena upande wa mashtaka waje na majibu.
Pia ameeleza kuwa wanaotakiwa kushtakiwa ni benki ya standard Chartered Hong Kong.
Aidha ameshangazwa kuona washtakiwa wengine wanaongezwa katika kesi hiyo, hivyo upelelezi hautakamilika kama watakuwa wanaongezwa na ili upelelezi ukamilike upande wa mashtaka wafuatilie nakala aliyowapelekea hao Takukuru.
Baada ya kusikia hoja hiyo hakimu Huruma Shaidi ameiahirisha hadi Febtuari 13, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Rugemarila wengine ni mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Seth, na mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege, ambaye aliunganishwa katika kesi hiyo Desemba 20 mwaka jana.
Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni pamoja na kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu , kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuisababishia serikali hasara na kutakatisha fedha.