The House of Favourite Newspapers

Rukia: nateseka jamani

0

Na Chande Abdallah
Rukia Kasende (63) mkazi wa Masasi, Mtwara ni mmoja wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam akisumbuliwa na maradhi ya saratani (kansa) ya kichwa ambayo yanamsababishia maumivu makali huku akikabiliana pia na changamoto ya kukosa fedha za matibabu na za kujikimu.

UGONJWA ULIVYOANZA
Akizungumza na mwandishi wetu, Rukia ambaye pia ni mlemavu wa ngozi (albino) alisema kuwa ugonjwa huo ulimuanza mwaka 2007 kama kipele ambacho kilikuwa kikiongezeka kwa kasi huku akipata maumivu makali ya kichwa.

“Kilianza kama kipele, kikawa kinauma sana mpaka maumivu yakawa ya kichwa kizima. Wakati huohuo uvimbe ukaanza kukua huku kidonda kikiendelea bila kupona.

“Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya ndipo nikaenda Hospitali ya Ndanda na ikashindikana matibabu. Nikaandikiwa kuja hapa Ocean Road na uvimbe ndiyo ukakua mpaka hivi unavyoniona,” alisema Rukia.

GHARAMA ZA MATIBABU
“Nimeambiwa inabidi nipasuliwe kichwa ili kuondoa uvimbe, gharama yake ni shilingi laki 8 na mimi sina kitu chochote, nateseka jamani, nisaidieni,” alisema Rukia huku akionesha kuwa kwenye maumivu makali.

Rukia aliongeza kuwa hana msaada wowote kwa kuwa mume wake aliuawa mwaka 2012 nyumbani kwake na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi huku akimwachia watoto watatu.

“Ninashindwa kabisa kufanya shughuli yoyote ya kuniingizia kipato maana hapo kabla nilikuwa nikijishughulisha na kilimo,” alisema Rukia.

AANDIKIWA MIONZI
Rukia aliendelea kueleza kuwa, baada ya kukaa muda mrefu bila kupata fedha hizo za upasuaji, madaktari waliamua kumuandikia tiba ya mionzi ambayo amekuwa akiitumia kwa muda wote wakati akisubiria upasuaji.

“Waliniandikia mionzi lakini kama unavyoona kidonda kimekuwa kikubwa, nikipigwa mionzi nazidi kuumwa, halafu wagonjwa wenzangu wodini wakawa wananisimanga kwamba naishi kwa kutegemea misaada,” aliongeza Rukia.

AONDOKA HOSPITALINI
“Kutokana na kukosa fedha za matibabu kamili, ukichanganya na manenomaneno ya wagonjwa wenzangu, nilimuomba dokta aniruhusu nitoke hospitali ili nikatafute fedha za kugharamia matibabu.

Akaniruhusu na kuniambia nirudi baada ya miezi mitatu, sasa hivi naishi kwa ndugu zangu Tegeta, Dar, hata nauli ya kurudia kwetu Masasi sina, naomba wasamaria wema mnisaidie, nakufa mwenzenu,” alihitimisha Rukia.

Kutoa ni moyo na kabla hujafa, hujaumbika! Kwa yeyote aliyeguswa na mkasa huu wa Rukia, atoe msaada wake kupitia namba 0675542382.

Leave A Reply