The House of Favourite Newspapers

Rungwe Aahidi Kujenga Daraja Dar Hadi Zanzibar

0

MGOMBEA urais kupitia chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), Hashim Rungwe, amesema akipata ridhaa ya kuongoza nchi katika uchaguzi mkuu ujao, atatumia siku ishirini za kwanza kugawa chakula kwa wanafunzi na wagonjwa hospitalini, kwani huko ndipo kwenye changamoto kwa sasa.

 

Ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chama hicho katika viwanja vya Manzese jijini Dar es Salaam.

 

Amesisitiza sera ya kuwapatia chakula wanafunzi shuleni, ili kusaidia kukuza uelewa kwa wanafunzi hao na kusaidia kundi kubwa la wanafunzi kutohudhuria madarasani kutokana na ukosefu wa chakula.

 

Vilevile, chama hicho kimeahidi kujenga daraja kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar ili wananchi waachane na usafiri wa meli na boti ambao kimesema siyo rafiki kwao.

 

Jana, katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho eneo la Manzese Bakhresa jijini Dar es Salaam, Rungwe hakutekeleza ahadi yake ya kutoa ubwabwa kwa wananchi kutokana na amri ya kupinga hatua hiyo kutoka  Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU).

 

Taasisi hiyo ilionya kuwa kutoa chakula kwa wananchi kipindi hiki cha kampeni ni kosa kwa mujibu wa sheria. Rungwe alisema jana kuwa alipanga kutoa ubwabwa kwenye mkutano, lakini TAKUKURU wamempiga marufuku.

 

Mgombea mwenza wa Rungwe, Mohamed Masoud Rashid, alisema sera za CHAUMMA ni bora kuliko chama kingine cha siasa nchini na mpango wao wa kupeleka bahari Dodoma wana imani utaporwa.

 

“Dodoma tangu itangazwe kuwa makao makuu ya nchi imechukua zaidi ya miaka 40 kuhamishia ofisi huko. Kwa hiyo, na sisi tumedhamiria kuipeleka bahari Dodoma ili kuunga juhudi hizo,” alisema.

 

Rashid pia alisema wananchi wakikipa ridhaa chama hicho, serikali yake itajenga daraja kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam ili kurahisisha usafiri.

Leave A Reply