RWANDA: Mwanahabari Akamatwa kwa Tuhuma za Ugaidi

MWANDISHI  wa habari wa kujitegemea wa Rwanda, Phocus Ndayizera, ameonyeshwa mbele ya vyombo vya habari na polisi wa upelelezi wiki moja baada ya kutoweka ambapo imedaiwa anatuhumiwa kwa makosa ya ugaidi.

Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la Uingereza (BBC), Yves Bucyana,  mwandishi huyo ambaye hufanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali ikiwemo BBC katika  idhaa ya Kinyarwanda na Kirundi,  amesema  hajui kwa nini amekamatwa.

Wiki moja baada ya kutoweka, mwandishi huyo amepatikana wakati alipoonekana mbele ya waandishi wa habari kwenye makao makuu ya idara ya polisi inayohusika na upelelezi akiwa amevaa pingu na hali yake ikionyesha alikuwa amechoka.

Mara ya mwisho kwa Ndayizera kuiandikia habari BBC ilikuwa mwezi wa sita mwaka huu.

Alipotakiwa na polisi kuwaambia waandishi wa habari tuhuma dhidi yake, Ndayizera alisema  hana habari yoyote kuhusu mashitaka dhidi yake akisisitiza tu kwamba na yeye anasubiri upelelezi kukamilika.

Amesema kwamba alikamatwa katika mtaa wa Nyamirambo jijini Kigali alipokwenda kumuona jamaa yake na kupelekwa sehemu isiyojulikana kabla ya kujikuta katika mahabusu ya polisi kituo cha Remera.

Msemaji wa idara ya upelelezi Modeste Mbabazi amewambia waandishi wa habari kwamba Ndayizera anatuhumiwa kwa kujihusha na ugaidi

Polisi wa upelelezi wamekiri kuwa ndiyo waliokuwa wanaomshikilia mwandishi huyo kwa wiki nzima.

Mbabazi amewambia waandishi wa habari kwamba Ndayizera anatuhumiwa kwa kujihusha na ugaidi na pia kukutwa na vifaa vya vilipuzi.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, walikuwa na taarifa za mipango ya watuhumiwa kutumia vilipuzi kuhatarisha usalama wa nchi ya Rwanda.

Toa comment