The House of Favourite Newspapers

Saa 48 simu feki kuzimwa, TCRA hawakwepi mzigo wa lawama

0

TCRA (1)JUNI 16, mwaka huu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) itazima simu zote ambazo ni feki, kufuatia kumalizika kwa muda uliotolewa ili kuhakikisha soko linabakia na bidhaa zenye ubora na viwango vilivyoainishwa.

Ingawa lengo la serikali katika kuchukua hatua hii ni jambo zuri, lakini lazima tuwe wakweli kuwa wananchi wanabebeshwa mzigo ambao ulitokana na uzembe wa mamlaka zinazohusika na bidhaa za mawasiliano.

Kwa mfano, lilikuwa ni jukumu la TCRA kuhakikisha soko la ndani haliwi na bidhaa feki katika mzunguko wake kwa sababu jambo hili lingewezekana kufanyika mapema kama inavyotaka kufanya sasa.

Serikali inafahamu kuhusu uingizwaji wa bidhaa hizi feki na baadhi ya waingizaji ni wafanyabiashara wakubwa wanaofahamika, pamoja na mitandao ya simu yenye majina makubwa.

Na sekta hii ya mawasiliano imekuwa kubwa na iliyorahisisha mambo mengi sana katika miaka ya karibuni kwani kama tunavyojua, hivi sasa wenye kumiliki simu za mikononi ni wengi, kwani wamesambaa hadi vijijini kabisa, eneo ambalo miaka michache nyuma, lilikuwa gumu mno kufikiwa kimawasiliano.

Katika zoezi hili la uzimaji simu, waathirika wengi ni watu wa vijijini, kwani wafanyabiashara wasio waaminifu waliwalenga wao zaidi.

Inakadiriwa zaidi ya simu milioni sita zitaondoka sokoni, kitu kinachoashiria kuwa mamilioni ya shilingi za Watanzania zitakuwa zimeyeyuka, hasa ukizingatia kuwa wapo baadhi ya watu walinunua hadi simu za shilingi 700,000 na wengine 1,000,000.

Wote tunajua jinsi maisha yalivyo magumu, hasa upatikanaji wa fedha. Kila kitu kipo juu kuanzia vyakula, huduma muhimu kama afya, elimu, usafiri na hata kilimo, vyote hivyo vinahitaji fedha ili mtu aweze kumudu.

Sasa leo unapomzimia mtu simu yake aliyonunua hata kwa elfu hamsini, maana yake unamlazimisha atafute hela nyingine ili anunue nyingine, kitu ambacho kinamuumiza mno kwa vile analazimika kubeba mzigo uliosababishwa na serikali yenyewe.

Kwa jinsi mawasiliano yalivyo na umuhimu, nafikiri serikali inalo jambo inatakiwa kufanya ili kuwatetea wanyonge wanaoadhibiwa kwa kosa lisilo lao. Mojawapo ya jambo ambalo lingefanyika ni kudhibiti bidhaa zote feki za mawasiliano zisiingie tena na hizi zilizopo, zingepotea zenyewe sokoni taratibu.

Vinginevyo wananchi wanayo haki ya kudai fidia kwani TCRA ilishindwa kutimiza wajibu wake sawasawa wakati ikifahamu kuwa bidhaa feki hazitakiwi. Kama leo imeweza kuzima simu zisizo na viwango ni wazi kuwa uwezo huo ulikuwepo huko nyuma, lakini ama kwa kufaidika au kwa makusudi, iliacha kuchukua hatua stahiki.

Waagizaji na wauzaji wa simu feki ni miongoni mwa makampuni makubwa ya simu, ambayo watu waliyaamini kwa vile yaliziuza madukani mwao, sasa leo unapomuadhibu mnunuzi na kumuacha muuzaji ni dhuluma ya wazi na safu hii inakemea hilo!

Nachochea tu! 

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave A Reply