The House of Favourite Newspapers

Sababu 4 Matajiri CCM Kutompa Uenyekiti JPM

0

magufulikijanRais Dk. John Pombe Magufuli.

Na MWANDISHI WETU, RISASI MCHANGANYIKO

DAR ES SALAAM: Wakati mkutano mkuu wa dharura wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukitarajiwa kufanyika Jumamosi hii mjini Dodoma, sababu tano za kwa nini matajiri ndani ya chama hicho hawataki Rais Dk. John Pombe Magufuli apewe chama zimefichuka.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli anatarajiwa kukabidhiwa kofia ya uenyekiti wa chama hicho tawala, kutoka kwa mwenyekiti wake wa sasa, Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ikiwa ni mwendelezo wa utamaduni wa kuachiana nafasi hiyo kabla ya muda.

Chanzo ndani ya CCM kimelidokeza gazeti hili kuwa sababu ya kwanza, ni kuwa viongozi wengi, hasa wenyeviti wa mikoa, ni wafanyabiashara matajiri, ambao wana hofu ya kuondolewa kwenye nafasi zao, kwa kuangalia utendaji wa Rais Magufuli ndani ya serikali.

“Katika nafasi zao nyeti kwenye chama, matajiri hawa walikuwa na uwezo wa kujua mipango ya serikali na kuweza kujihami au kuzuia, wakiondolewa kwao itawawia vigumu, ndiyo maana wanapambana mwanzo mwisho,” kilisema chanzo hicho.

Kiliitaja sababu ya pili kuwa ni hofu yao ya kugusika kirahisi, wakiwa hawana ukubwa ndani ya chama. “Wakiwa na nyadhifa, baadhi za mamlaka ziliwahofia kuwagusa hasa katika mambo kama kodi kwenye biashara zao, lakini wakiondolewa, watafikiwa kirahisi,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo chetu kiliitaja sababu ya tatu inayowafanya matajiri hao kuhaha usiku na mchana kuzuia kofia asipewe JPM ni kuwa endapo watapokwa nafasi zao, watapoteza baadhi ya upendeleo waliokuwa wakiupata katika masuala mbalimbali.

“Unajua kwa nafasi zao, hawa jamaa walikuwa wanapata upendeleo sehemu nyingi, kitu kilichokuwa kinawavutia hasa kwa sababu ya utajiri wao, walikuwa wanaweza kukutana na mkubwa yeyote serikalini, sasa wakiondolewa, ni pigo kubwa kwao, hawataki hata kidogo huyu jamaa apewe chama, wanamjua, atawang’oa tu,” kilisema chanzo hicho.

Licha ya sababu hizo, nyingine kubwa kinachowapa hofu matajiri ambao ni viongozi ndani ya chama tawala ni kufilisiwa, kutokana na wengi wao kutolipa kodi stahiki na kwa wakati.

“Katika kodi, JPM hataki mchezo na wao wanajua, kwa miaka mingi viongozi wa chama wamekuwa hawalipi sawasawa au hawalipi kabisa, sasa serikali ya awamu ya tano imeanza makeke yake, kuna watu wanalazimika kulipa malimbikizo.

“Wanajua wakivuliwa nyadhifa zao, kitakachofuata ni kufilisiwa utajiri wao, kitu ambacho hawataki kabisa kukiona, hawa ndiyo wanaokesha usiku kucha wakitafuta mbinu za jinsi gani ya kumzuia JPM kupewa chama,” kilisema chanzo chetu.

Katika historia ya CCM, ni Mwalimu Julius Nyerere pekee ndiye aliyemaliza kipindi chake chote cha uenyekiti, baada ya kung’atuka urais mwaka 1985, kwani alikalia nafasi hiyo hadi mwaka 1992 muda wake ulipoisha.

Waliomfuatia, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete wamekuwa wakiachia nafasi hiyo kila baada ya kumaliza muhula wao wa miaka kumi ya urais,  ambao humalizika miaka miwili kabla ya uchaguzi wa chama kwa mujibu wa katiba.

Leave A Reply