Sababu Harmonize Kufuta Shoo Majuu

MSANII mwingine mkali anayeiwakilisha Bongo Kimataifa, Harmonize au Konde Boy Mjeshi amelazimika kufuta na kuahirisha ziara yake ya muziki katika nchi ya Canada na Uswisi ambapo meneja wake amefunguka sababu ya yote hayo.

 

Konde boy alikuwa amepanga kuwatumbuiza mashabiki wake huko Canada mnamo Oktoba 30, mwaka huu na nchini Sweden, Novemba 6, mwaka huu, lakini ziara yake imeahirishwa.

 

Akizungumzia na Gazeti la IJUMAA kuhusu ishu hiyo, mmoja wa mameneja wa Harmonize, Beauty Mmary au Mjerumani amesema;

 

“Kwanza tunamshukuru Mungu tangu tumefika Marekani tumeshafanya shoo tatu na mapokezi yalikuwa mazuri sana.

 

“Kwetu sisi tumechukulia kwamba soko letu sasa hivi limekuwa kwa sababu muziki wetu unasikilizwa.

 

“Naomba niwakumbushe kwamba shoo za Harmonize zimeandaliwa na mapromota na ndiyo wao wanafanya promosheni, lakini hata sisi tunafanya kwa kuwa tumeshafika hapa Marekani,” amesema Mjerumani na kuongeza kuwa kusitishwa au kuahirishwa kwa shoo za Harmonize za Canada na Uswisi ni kutokana na sheria kali zilizowekwa kwenye nchi hizo kutokana na udhibiti wa kusambaa kwa Virusi vya Corona au UVIKO-19.

 

“Hali inavyoendelea wanaona labda mkusanyiko wa watu ni hatari hivyo ni jambo ambalo lipo nje ya uwezo wetu kutokana na vizuizi walivyoweka.

 

“Ni kweli tunatamani sana wasanii wetu wafanye shoo kote huko, lakini ndiyo imekuwa hivyo hawaruhusu mikusanyiko kutokana na ongezeko la wagonjwa.

 

“Hata hivyo, kwa Ulaya, kama watawahi kufungua na kuruhusu mikusanyiko kwa kuwa tupo huku hadi Desemba tutakwenda kufanya tu bila shida yoyote,” anasema Merumani.

 

Harmonize au Harmo ambaye ameambatana msanii wake, Ibraah nchini Marekani, wanaendelea na shoo za kimataifa nchini humo.

 

STORI; KHADIJA BAKARI, DAR


Toa comment