The House of Favourite Newspapers

Sababu Mpya kwa Nini Wanaume Wengi Hawaoi Siku Hizi?

0

RAFIKI, kumekuwa na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa jamii kwamba imekuwaje vijana wa kiume wamekuwa ni waongo hasa linapokuja suala la kuoa?

Kwa kadiri siku zinavyokwenda ndivyo ambavyo idadi ya wanaume wanaoogopa kuoa inazidi kuongezeka.

Utakuta wapenzi wanaambiana kwamba wanapendana na kuahidiana kuwa wataoana, lakini kitakachotokea baada ya hapo ni mwanaume kuanza kupiga chenga kwa visingizio lukuki.

Ukweli ni kwamba hakuna jibu la moja kwa moja juu ya tatizo hilo, lakini zipo sababu mpya ambazo walau zinatoa tafakuri;

Ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano; hapa nawazungumzia wale watoto wa kiume waliolelewa malezi ya upande mmoja; yaani walilelewa na mama peke yao.

Sina maana ya kudharau au kutweza malezi ya mama, la hasha, lakini ni vyema mkafahamu kwamba kuwa na baba asiye na malezi mazuri si sawa na kutokuwa na baba. Na ndiyo maana nikasema ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano.

Achilia mbali aina ya malezi atakayoyapata kwa familia yawe mazuri au mabaya, lakini lazima kutakuwa na tabia za kiume zitakazoakisi malezi ya mtoto wa kiume kwenye familia husika.

Watoto waliolelewa na mama peke yao kuna kitu huwa wanakosa, kwani wanakuwa hawana mtu wa kumchukulia kama mfano kwa upande wa jinsi ya kiume na hapo ndipo hujikuta wakijifunza wenyewe namna ya kuongea na kutenda kama wanaume kwa sababu katika makuzi yao hawakupata fursa ya kuwa karibu na baba zao.

Kwa kuwa siku hizi kuna kundi kubwa la akina mama ambao wamejikuta wakiachiwa mzigo wa malezi ya watoto, baada ya aidha kuachwa na waume zao au kuzalishwa na kutelekezwa (single mothers) na hapo ndipo tunaposhuhudia mtoto wa kiume anapokua kwa umri na kimo huku akiwa hana mtu wa kumuangalia kama mfano wa mume.

Wanaume waliopitia malezi ya aina hii huchelewa kuoa kwani huyaangalia maisha ya ndoa kwa namna ya kujaribu na ndipo hapo wengi huishia kuishi kinyumba na wanawake kwa ajili ya kutaka kujifunza namna ya maisha ya ndoa yanavyotakiwa kuwa na ndiyo sababu huchukua muda mrefu kufanya maamuzi.

Kuna migogoro mingi ya kiuchumi; kuna kundi kubwa la vijana siku hizi hawana ajira au hawana uhakika na kipato. Ukweli ni kwamba hakuna mwanaume atakayependa kujiingiza kwenye ndoa wakati hana kazi au uhakika na kipato chake.

Na hiyo ni kutokana na wanawake wengi siku hizi kuonekana kujali zaidi wanaume wenye uhakika na kipato. Hii misemo ya wanawake ya kebehi dhidi ya wanaume wasio na ajira au kipato, kama vile ‘mwanaume suruali’ ina mchango mkubwa kwenye kuwafanya wanaume kukwepa kuoa kama hawana ajira au hawana uhakika na kipato chao.

Kiwango cha elimu ya juu; siku hizi wanawake wengi wameibuka katika kutafuta elimu ya juu kwa juhudi kubwa. Idadi ya wanawake wanaojiunga na vyuo vikuu ni wengi tofauti na ilivyokuwa zamani. Na hiyo ni kutokana na wazazi wengi kubadili mtazamo wao juu ya mtoto wa kike.

Zamani mtoto wa kike alichukuliwa kama kitega uchumi. Kwa maeneo ya vijijini na katika familia maskini, watoto wa kike walikuwa wanatazamwa kama ‘biashara ya kesho’ ambapo watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa hiyo thamani yao ilikuwa ni kuolewa, ni ile ya kibidhaa na siyo kibinadamu.

Lakini tofauti na zamani siku hizi hata vijijini kumekuwa na mwamko mkubwa wa kumsomesha mtoto wa kike hadi elimu ya juu. Kutokana na mwamko huo wanawake wengi wamejikuta wakiona elimu kama kimbilio pekee la kuepukana na mfumo dume.

Wanaume huwaona wanawake kama tishio wanapokuwa na mafanikio makubwa kippesa; inaweza kutokea mwanaume anaweza kuwa na uhusiano na mwanamke ambaye labda tu nisema ni mbangaizaji.

Wakati huo anaweza kuahidi kufunga ndoa na mwanamke huyo, lakini iwapo itatokea mwanamke huyo akapata mafanikio kibiashara na kuinuka kipesa. Kama mwanamke asipokuwa makini anaweza kusababisha mwanaume huyo akaingia mitini. Sababu kubwa hapo inaweza kuwa ni hofu ya kuogopa kuongozwa na mwanamke.

Wanaume wengi siku hizi wana hofu ya majukumu, hasa ya kulea watoto; kutokana na malezi yao au kile wanachokijua kuhusu watoto, baadhi ya vijana huamini kwamba, kulea watoto ni jambo gumu. Lakini wengine wanaamini kwamba, hata mke anapaswa kulelewa kama ilivyo kwa mtoto.

Hivyo wanaamua kutafuta kwanza uwezo ambao haupatikani kirahisi. Kuna wengine, ambao wamefundishwa au kuelekezwa na mila na desturi zao kwamba, kabla hawajaoa, ni lazima wawe na nyumba kwanza, tena kwao. Kwa hiyo, hawa hadi waje wapate uwezo wa kipesa wanakuwa wameshachelewa.

Kuna baadhi ya wanaume, maisha bila ya ndoa wanayaona kuwa ndiyo bora kuliko yale ya ndoa; kuna baadhi ya wanawake hujirahisisha kwa wanaume. Siku hizi ni jambo la kawaida kukuta mwanaume anaishi na mwanamke bila ndoa.

 

Na hapo ndipo unapokuta wanaume hawaoni tena umuhimu wa kuoa. Sasa kama mwanamke anaweza tu kuishi na mwanaume bila ndoa na mwanaume huyo akapata huduma zote kutoka kwa mwanamke huyo, unadhani ni kitu gani kitamvuta kufunga ndoa?

 

Jambo lingine ni ile dhana kwamba maana ya ndoa ni tendo la ndoa. Siku hizi wanaume wengi wamejikuta wakiwa hawahitaji tena kuoa kwa sababu tendo hilo linapatikana kirahisi tofauti na zamani. Siku hizi inawezekana kumtongoza binti leo na kupata tendo siku hiyohiyo.

Leave A Reply