The House of Favourite Newspapers

Sababu Sita za Kutekwa Mohammed Dewji

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Kangi Lugola.

SERIKALI ya Tanzania, imetaja mfano wa sababu sita za jumla ambazo zinaweza kuwa chanzo cha kutekwa Mohammed Dewji ambaye ameibua taharuki ndani ya Simba na Tanzania kwa ujumla.

 

MO amekuwa msaada mkubwa wa kiuchumi ndani ya Simba na tangu atekwe na watu wasiojulikana Alhamisi alfajiri ameibua sintofahamu kila kona ndani ya nchi.

 

Simba wanahofi a kutoweka kwa MO kutokana na mapenzi yake kwa klabu hiyo pamoja na kubeba sehemu kubwa ya gharama za klabu msimu huu kama mwekezaji.

Mohammed Dewji

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Kangi Lugola amewaambia waandishi wa habari jana Jumamosi jijini Dar es Salaam kwamba bado wanaendelea na upelelezi wa kina wa kutekwa kwa mwanachama huyo mtiifu wa Simba. Aliongeza pia katika upelelezi wao wanawashikilia watu 20 kwa uchunguzi na akaamuru kwamba kama kuna ambaye watajiridhisha kuwa hana hatia aachiwe arudi uraiani ndani ya saa 24.

 

Alisisitiza kuwa katika watu wanaowashikilia kuhusiana na sakata hilo hawezi kuwaweka wazi kwa
vile atavuruga upelelezi. “Zipo sababu nyingi ambazo zinapelekea mtu kutekwa.

 

Zingine ni za kisiasa, kiuchumi, ushirikina, mapenzi, visasi na kudhulumiana,”alisema Lugola ambaye ni mpelelezi aliyebobea. “Kiuchumi inaweza kuwa watu wana njaa wanaona wakimteka mtu mwingine watapewa kiasi fulani cha fedha kwa vile ana hela,”alisema Kangi mwenye miaka 55. Alisisitiza kwamba kwenye ishu ya MO na zingine zinazohusiana na utekaji taarifa rasmi itatolewa na jeshi la polisi na si watu wengine.

 

Kangi alisema kwamba polisi wanaendelea kumtafuta MO popote alipo ingawa hakuwa tayari kuweka wazi kama uchunguzi wao umebaini bado yupo ndani ya ardhi ya Dar es Salaam au la.

 

KINA MANJI WAPEWA ANGALIZO

Kangi pia aliwataka wafanyabiashara wakubwa na watu maarufu kuwa makini na suala la ulinzi wao binafsi kwani ni muhimu kwa usalama wao. “Suala la kujihakikishia usalama binafsi ni jambo muhimu sana kwa hawa watu,”alisema Kangi ambaye ni Mbunge wa Mwibala tangu mwaka 2010. Mashabiki hususani wa Simba wamekuwa wakijiuliza kuhusiana na kama MO alikuwa na ulinzi binafsi au la ingawa habari za awali zinadai kwamba alivyotekwa hakuwa na mlinzi alikuwa mwenyewe.

 

Kauli hii ya Lugola ina maanisha kuwa matajiri wengine wakubwa hapa nchini akiwemo Yusuf Manji ambaye amewahi kuwa mfadhili na kiongozi wa Yanga wanatakiwa kujiwekea ulinzi wa kutosha ili kuepuka kukumbwa na hali kama hii ya Mo.

STORI: SWEETBERT LUKONGE, SPOTI XTRA

Comments are closed.