The House of Favourite Newspapers

SABABU WANAWAKE KUUAWA ZAANIKWA

MATUKIO ya wanandoa kuuana yanaendelea kukithiri nchini na kuleta tishio jipya hasa kwa wanawake ambao kwa kiasi kikubwa ni waathirika wa matukio haya ya kinyama.  Risasi Jumamosi hivi karibuni limechimba kwa undani na kuibuka na sababu za wanaume ambao wanatajwa kuwa vinara wa mauaji ya wake zao, kufanya hivyo.

TAKWiMU HAZIONGOPI

Kwa mujibu wa takwimu kutoka jeshi la polisi zilizowahi kutolewa na msemaji wa jeshi hilo (si msemaji kwa sasa) mwaka 2017, Barnabas Mwakalukwa, zinaonesha kuwa wanaume wanaongoza kwa kufanya mauaji kwenye ndoa. Takwimu hizo zilionesha wanaume waliouawa na wake zao mwaka 2016/2017 ni 37 hadi kipindi cha mwezi Mei, huku wanawake waliouawa idadi yao ikiwa ni 133 katika kipindi hicho.

SABABU ZA MAUAJI

Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2017 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), inaonesha kuwa asilimia 16 ya matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yanasababishwa na wivu wa mapenzi.

Aidha, kichocheo kikuu cha wivu kwa mujibu wa uchuguzi wetu kinatajwa kuwa ni uwepo wa wapenzi wa pembeni maarufu kama michepuko, mawasiliano ya simu yasiyofaa kati ya wanandoa na watu wengine pamoja na matumizi yenye kutia mashaka kwenye mitandao ya kijamii.

MASWALI YALIYOIBUA TAFAKURI

Aidha, baada ya kuwepo mwendelezo wa mauaji kwa wanawake likiwemo tukio bichi la hivi karibuni la Naomi Marijani mkazi wa Kigamboni, Dar kudaiwa kuuawa na mumewe kisha mwili wake kuchomwa moto na mabaki kuzikwa, uchunguzi wa Risasi Jumamosi ulijikita katika kujiuliza yafuatayo: “Kama ni usaliti baadhi ya wanaume na wanamke wanatajwa kufanya; kwa nini wanaoumizwa zaidi kiasi cha kuamua kuua ni wanaume?”

“Wanaume wengi wanamiliki simu na mitandao ya kijamii na kuna wakati wanazitumia vibaya; kwa nini wanawake hawakasirishwi kiasi cha kuamua kuua?” “Migogoro kwenye ndoa huchangiwa na upungufu katika pande mbili, kwa sababu gani wanaume ndiyo wamekuwa vinara wa mauaji?”

SABABU WANAWAKE KUUAWA HIZI HAPA

Mwanasaikolojia mahiri nchini, Chris Mauki katika mazungumzo yake na Risasi Jumamosi hivi karibuni alisema, sababu ya msingi inayochangia wanaume kuua zaidi wenza wao ni kuendelea kuishi kwa kuuamini mfumo dume. “Mambo mengine yote, sababu nyingine zote unaweza kuziweka kwenye kapu hili, wanaume wengi huamini kwamba wao ni bora kimamlaka kuliko wanawake.

“Hivyo linapokuja suala la kusalitiwa huumizwa zaidi kwa sababu huhisi wenza wao wamedharau mamlaka zao, jambo ambalo huleta msukumo wa hasira kali. “Katika kuonesha kwamba wao wana nguvu na mamlaka kuliko wake zao huamua kutoa adhabu kama kupiga na wakati mwingine ndiyo hayo mauaji yanatokea,” alisema Mauki.

SABABU NYINGINE NI HII

Mwanasaikolojia mwingine nchini, Grace Makani wa kampuni ya ushauri kwa wanandoa na familia ya Grace Inc, akikaririwa hivi karibuni alipozungumza na chombo kimoja cha habari nchini, alisema kuwa chanzo kingine cha wanaume kufanya mauaji kwa wanawake ni mageuzi ya kiuchumi waliyofikia wanawake.

“Zamani mwanamke alikuwa mama wa nyumbani, kila kitu analetewa hivyo kujiamini kwake kimaisha kulikuwa kidogo. “Leo hii mwanamke wa miaka hiyo hayupo, mwanamke wa leo ni  Alisema wanawake wanaposalitiwa huwa wepesi kufungua mlango wa kusamehe tofauti na wanaume ambao hutajwa kuwa ni wagumu kufanya hivyo.

Mtazamo huu unakazia kwamba kile ambacho kimesemwa na wanasaikolojia wengi kuwa ‘Wanaume wengi wanajitukuza sana mbele ya wanawake.’ Wakati mwingine hata kama hawana sababu za kufanya hivyo.

NINI KIFANYIKE?

Ili kupunguza au kukomesha vitendo vya wanaume kuua wake zao elimu ya familia inahitajika kutolewa kwa upana ili kuwafanya wanaume waondokane na mtindo wa kutumikia mfumo dume.

Hata hivyo, wanawake nao wanapaswa kushauriwa kuchukua tahadhari hasa pale wenza wao wanapowaona kuwa wamebadilika kitabia kwa kuondoa mashaka yaliyopo kwao na kujenga upya msingi wa ndoa wa upendo na kusameheana. Aidha, juhudi kutoka kwenye mashirika ya dini, taasisi zinazojihusisha na masuala ya kijamii zinapaswa kuwepo katika kujenga familia zenye upendo na usawa.

KAZI YA VYOMBO VYA USALAMA KATIKA HILI

Katika hatua nyingine vyombo vya usalama hasa polisi vinao wajibu kuchukua hatua za kulinda matukio ya mauaji kwenye ndoa yasitokee kwa kushughulikia taarifa zote za vitisho zinazopelekwa vituoni na wenza.

Aidha, jeshi la polisi linapaswa kuwa mshauri wa masuala ya kifamilia na msimamizi mkuu wa haki pale linapokuja suala la vitisho vya mauaji na mauaji yenyewe kwa wahusika kuelimishwa au kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

WANAWAKE WALIOUAWA

Baadhi ya wanawake ambao wamedaiwa kuuawa na waume zao kwa sababu mbalimbali nchini na misiba yao kuhuzunisha wengi ni pamoja na ambao picha zao zimetumika ukurasa wa mbele wa gazeti hili. Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi- Amina.

Comments are closed.