The House of Favourite Newspapers

SABABU ZA WAJAWAZITO KUUMWA TUMBO KILA MARA

WAJAWAZITO wengi huugua wakati wakiwa na ujauzito na zipo sababu zinazofanya kutokea kwa maumivu ya tumbo wakati wa miezi mitatu ya kwanza ya mimba.  Kuna matatizo mengi ambayo yanahusiana tu na mimba. Maumivu ya tumbo kwa mjamzito ni changamoto kwa sababu wengi hupatwa na kichefuchefu, kutapika na maumivu ya tumbo hujitokeza mara nyingi. Mfuko wa uzazi unapotanuka unaweza kusukuma viungo vingine kando ndani ya tumbo.

Upungufu wa damu na leukocytosis ni kawaida katika mimba na si viashiriwa vya upungufu wa damu au maradhi. Kiinitete kinapojipandikiza katika kuta za ndani za mfuko wa uzazi kinaweza kusababisha maumivu ya tumbo, ambayo huchukua muda wa siku mbili au tatu na kiasi kidogo cha damu ukeni hutoka.

Mara nyingi kiasi hiki cha damu huwa ni kidogo na hutokea kati ya siku saba au 12 baada ya tarehe inayohisiwa mimba kutungwa, mara nyingi kipindi hiki hukaribiana na siku ambayo mwanamke alikuwa anatarajiwa kuingia hedhi. Hivyo, wagonjwa mara nyingi hufanya makosa kwa kufikiri kuwa wameingia katika siku zao kama kawaida. Mimba iliyotunga nje ya mfuko husababisha maumivu kwa akina mama wengi walio na mimba nje ya mfuko wa mimba.

Tatizo hili linaweza kubainika kwa kutumia Ultrasound na kipimo cha homoni cha HCG, uzuri ni kwamba tatizo hili linatibiwa kama dharura kwa mama kufanyiwa upasuaji.

Ieleweke mimba inaweza kutoka yenyewe au kutolewa kwa makusudi. Tatizo hili huambatana na maumivu pamoja na kuvuja damu. Utoaji wa mimba usiokuwa salama unaongoza kusababisha vifo vya akina mama katika nchi zinazoendelea. Tatizo lingine ni uvimbe kwenye mirija ya mayai (Ovarian cyst) ambapo huweza kupasuka au kujizungusha.

Hata hivyo, unaweza kupungua na usipopungua unaweza kuondolewa kwa njia ya upasuaji hasa wakati wa muhula wa pili wa ujauzito. Kujizungusha kwa mirija ya mayai (Ovarian torsion) hujitokeza mara chache. Uvimbe kwenye mfuko wa uzazi pia husababisha maumivu hasa unapokuwa mkubwa.

Tatizo hili linaweza kusababisha ujauzito kutoka hasa katika miezi ya awali. Tatizo lingine ni la kidole tumbo (Appendicitis). Kidole tumbo hujitokeza kwa uwiano sawa kama wanawake ambao hawana ujauzito. Matibabu ya ugonjwa huu ni upasuaji.

Wengine hupata mawe kwenye mfuko wa nyonga lakini pia kutokana na mabadiliko ya homoni wanawake wengi hupata tatizo la mawe kwenye mfuko wa nyongo.

Tatizo hii huweza kugunduliwa kwa njia ya kupimwa na kipimo cha Ultrasound na matibabu yake hutegemea na dalili alizonazo mgonjwa. Uvimbe kwenye mfuko wa nyongo ni tatizo la ghafla linalosababisha maumivu makali ambalo pia hujitokeza wakati mwanamke ana mimba.

Tatizo hili mara nyingi husababishwa na mawe kwenye mfuko wa nyongo. Matibabu yake hutumika dawa za kuua bakteria yaani Antibiotics. Lipo pia tatizo la wanawake wengi wakati wa ujauzito kupata maambukizi kwenye njia ya mkonjo mara kwa mara. Hii ni kutokana na mabadiliko yanayojitokeza wakati wa mimba. Sababu nyingine ya maumivu husababishwa na Round Ligament.

Ligament hii ndiyo inayoshikilia mfuko wa uzazi. Mfuko wa uzazi unavyozidi kukua, ligament hii huvutika na kusababisha maumivu ya tumbo. Dawa za maumivu husaidia tatizo hili. Ultrasound hutumika katika uchunguzi wa maumivu ya tumbo wakati wa ujauzito.

TIBA NA USHAURI

Uonapo maumivu yoyote kwenye tumbo kama wewe ni mjamzito, wahi kamuone daktari ili ajue tatizo na kukupa tiba.

Comments are closed.