Wiki hii safu hii inamleta kwenu mrembo Sabrina Omary ‘Sabby Angel’ (23) ambaye ni mwigizaji wa sinema za Kibongo.
Anaishi Kimara-Mwisho jijini Dar na dada anayemsaidia kazi za nyumbani. Ana mtoto wa kiume aitwaye Sameer aliyezaa na mwanaume ambaye hayupo naye kwa sasa na hapendi kumzungumzia.
Ungana nami kujua mambo mengi kuhusiana na mrembo huyo:
Mpaka Home: Vipi Sabby unapenda kuishi maisha ya namna gani?
Sabby: Napenda maisha ya kawaida lakini yanipe furaha na sababu ya kuishi.
Mpaka Home: Ni kitu gani ambacho huwa hakikosi kwenye jokofu lako?
Sabby: Napenda sana kuweka juisi hata madumu mawili.
Mpaka Home: Kila mtu ana nguo yake anapenda kuivaa wakati anapokuwa nyumbani kwa upande wako unapenda kuvaa nini?
Sabby: Napenda sana kuvaa dera, nguo ambayo ni pana inayonipa uhuru.
Mpaka Home: Mastaa wengi huwa wanaogopa kuingia jikoni wanaona kama watafubaa uso vipi kwa upande wako?
Sabby: Mimi hata ukiangalia kucha zangu sibandiki hata siku moja kwa ajili ya jikoni, niko vizuri sana kwa upande huo.
Mpaka Home: Kuna watu huwa kitanda ni popote, vipi wewe umeshawahi kulala sebuleni?
Sabby: Sana tu kuna wakati unaangalia filamu unapitiwa mpaka asubuhi na wakati mwingine unagombana na mpenzi (hakumtaja jina) unaenda kulala sebuleni.
Mpaka Home: Ni chakula gani unapenda kumuandalia mgeni anapokuja kwako?
Sabby: Pilau, naona wengi wanapenda chakula hicho.
Mpaka Home: Ni picha gani ambayo ikikosekana sebuleni kwako unahisi pamepwaya?
Sabby: Picha ya mwanangu na ya mama yangu.
Mpaka Home: Nakushuru sana Sabby kwa ushirikiano wako.
Sabby: Karibu tena!