The House of Favourite Newspapers

SACHEZ ASEPA MAN U, ATIMUKIA INTER MILAN

MANCHESTER United imekubaliana na Inter Milan kuwapa straika Alexis Sanchez kwa mkopo wa msimu mmoja. Lakini Manchester United itapaswa kutimiza sharti la kubeba mzigo mzito wa kulipa zaidi ya nusu ya mshahara wa Sanchez katika kipindi chote atakachokuwa huko.

 

Sanchez alikuwa anatazamiwa kutua jana Jumatano jijini Milan ili kukamilisha dili hilo ambalo litamfanya acheze kwenye Serie A hadi Juni 2020. Staa huyo wa timu ya taifa ya Chile anapokea mshahara wa pauni 505,000 (Sh. bilioni 1.4) kwa wiki kutoka Manchester United.

 

Manchester United inatakiwa kulipa asilimia 60 ya mshahara wa Sanchez atakapokuwa Inter Milan. Hali hiyo sasa inaifanya Manchester United inayonolewa na Ole Gunnar Solskjaer kuzidi kuwa na uhaba wa mastraika.

 

Manchester United ina maana imebakiwa na mastraika watatu nao ni Marcus Rashford, Anthony Martial na kinda wa miaka 17, Mason Greenwood.

 

Klabu hiyo hivi karibuni ilimuuza Romelu Lukaku kujiunga na Inter Milan inayonolewa na Antonio Conte. Sanchez tangu amejiunga na Manchester United akitokea Arsenal mwaka 2018 amekuwa na rekodi mbovu. Alichezea Manchester United jumla ya mechi 45 lakini alipachika mabao matano tu.

Comments are closed.