The House of Favourite Newspapers

Sadifa Akwama Kortini, Arejeshwa Rumande Hadi Desemba 19

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Dodoma imesema itatoa uamuzi wa maombi ya dhamana Desemba 19,2017 kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis (Mbunge) anayekabiliwa na mashtaka ya kutoa rushwa wakati wa uchaguzi mkuu wa viongozi wa UVCCM Taifa.

 

Upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kiapo kuzuia dhamana kwa madai kuwa kuvuruga upelelezi na kuingilia uchaguzi wa UVCCM  ambao ulifanyika jana Jumapili, Desemba 10,2017 na leo Jumatatu katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, Mjini Dodoma.

 

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Biswalo Biswalo amedai Sadifa anashtakiwa kwa makosa mawili ambapo katika shtaka la kwanza amedai Desemba 9,2017 katika makazi yake kwenye Kata ya Mnada, Mjini Dodoma akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM na muajiri wa umoja huo aliwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja huo.

 

Sadifa katika shtaka la pili anadaiwa katika eneo hilo na siku hiyohiyo, aliwaahidi kuwalipia usafiri wanachama wa umoja huo kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi huo.

 

Biswalo amesoma hati ya kiapo iliyotolewa na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga kupinga maombi ya dhamana kwa sababu endapo atapewa dhamana atavuruga upelelezi na kuingilia uchaguzi wa vijana.

 

Wakili wa Utetezi, Godfrey Wasonga amepinga hoja hiyo akisema makosa aliyoshtakiwa nayo mteja wake yana dhamana na hawezi kuingilia uchaguzi kwa kuwa umeshafanyika na mshindi ametangazwa.

 

Kutokana na mabishano hayo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Emmanuel Fovo ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19,2017 kutoa nafasi ya mahakama kupitia kiapo kilicholetwa na upande wa mashtaka ili kutoa haki katika maombi ya dhamana ya mshtakiwa. Kutokana na hilo, Sadifa amerejeshwa rumande.

 

CREDIT: Mwananchi.

 

VIDEO YA MATOKEO HAYO IKO HAPA

Comments are closed.