Sadney Apewa Program Maalumu Yanga

BAADA ya kuonekana kutokuwa vizuri katika kuzifumania nyavu, mshambuliaji wa Yanga, Mnamibia, Sadney Urikhob ameandaliwa program kabambe ya kuhakikisha anakuwa fiti.

 

Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera amemwandalia Sadney program maalum ya kufanya ili kuhakikisha anakuwa fiti na bora katika kuzitumia nafasi za kufunga atakazokuwa anazipata. Tangu atue Yanga, Sadney amekuwa akikabiliwa na changamoto ya kuzitumia ipasavyo nafasi za kufunga ambazo amekuwa akizipata uwanjani jambo ambalo limekuwa likiwakera wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.

 

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo Championi Jumatatu limezipata zimedai kuwa baada ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting ambao Sadney alikosa nafasi nyingi za kufunga, Zahera aliamua kumpatia program hiyo ambayo tayari ameshaanza kuifanyia kazi mazoezini.

 

“Zahera kwa sasa anataka timu ifanye vizuri, amewaambia washambuliaji wabadilike na wahakikisha wanazitumia ipasavyo nafasi za kufunga wanazokuwa wanapata hususani Sadney ambaye tayari amepewa program maalum ya kuhakikisha anakuwa sawa,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Alipoulizwa kuhusiana na hilo Zahera alisema: “Tunahitaji ushindi katika mechi zetu zijazo kwa hiyo yale yote yaliyojitokeza katika mechi zetu zilizopita tayari nimeshayafanyia kazi.

 

“Kuhusiana na Sadney kuna program maalum ambayo yeye pamoja na washambuliaji wengine wanafanya kwa sasa ili kuhakikisha wanakuwa fiti na makini zaidi katika kuzitumia nafasi za kufunga watakazokuwa wakipata uwanjani,” alisema Zahera.

Hata hivyo, tangu Sadney atue Yanga rekodi zinaonyesha kuwa timu hiyo imefanikiwa kucheza mechi 14, 11 kati ya hizo ni za kirafiki, mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya ligi kuu.

 

Katika mechi hizo, Sadney amefanikiwa kufunga mabao mawili kwenye mechi za kirafiki.

Washambuliaji wenzake ambao amekuwa akianza nao katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo mara kwa mara ambao ni Mganda, Juma Balinya pamoja na Mnyarwanda, Patrick Sibomana wao wamekuwa wakionekana kufanya vizuri.

 

Katika mechi hizo Sibomana amefanikiwa kufunga mabao saba, sita akifunga kwenye mechi za kirafiki na moja katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Upande wake, Balinya yeye amefunga mabao sita, matano akifunga katika mechi za kirafiki na moja kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam


Loading...

Toa comment