Said Ndemla Ruksa Kutua Yanga SC

IMEVUJA! Ndivyo utakavyoweza kusema ni baada ya Simba kupanga kuachana na kiungo wao, Said Ndemla mwishoni mwa msimu huu.

 

Kiungo huyo ambaye hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha Kocha Mbelgiji Sven Vandenbroeck na ni kati ya wachezaji wanaotarajiwa kumaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu, hiyo ikiwa na maana kuwa anaweza kuruhusiwa kwenda hata Yanga ambako amewahi kuhusishwa mara kadhaa.

 

Wengine wanaomaliza mikataba yao ni Hassan Dilunga, Yusuf Mlipili, Paul Bukaba, Mohammed Ibrahim, Deo Kanda, Sharraf Eldin Shiboub na Pascal Wawa.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kocha Sven ndiye aliyetoa mapendekezo ya kuachana na kiungo huyo ili aende akapate nafasi ya kucheza sehemu baada ya kuikosa Simba.

 

Mtoa taarifa huyo aliongeza Ndemla anakosa nafasi ya kucheza kutokana na ushindani wa namba uliokuwepo katika msimu huu huku wakipanga kusajili viungo wengine wenye uwezo mkubwa zaidi yake.

“Sasa muda muafaka wa Ndemla kuondoka Simba baada ya kudumu kwa muda mrefu huku akiwa hana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Sven.

 

“Kocha huyo amepanga kuachana na wachezaji wote wasiokuwa na faida kwa maana ya wale wasiokuwa na nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na lengo lake kuwaleta wengine watakaoleta changamoto ya ushindani wa namba katika timu.

 

“Hivyo, Ndemla ni lazima ataondoka baada ya msimu huu utakapomalizika ni baada ya kudumu kwa muda mrefu katika timu bila ya mafanikio ya kupata nafasi ya kucheza katika timu,” alisema mtoa taarifa.

Katibu Mkuu wa Simba, Anorld Kashembe alizungumzia hilo kwa kusema: “Bado muda wa usajili haujafika, hivyo ni vema tukasubiria muda utakapofikia hivi sasa akili za viongozi na wachezaji yapo kwenye ubingwa wa ligi kuu.”

 

NIYONZIMA AMPA SOMO NDEMLA

Kiungo mchezeshaji wa Yanga, Haruna Niyonzima amemtaka Ndemla kutafuta changamoto mpya nje ya Simba ili kuboresha makali yake.

“Ndemla ni mchezaji mzuri, unajua Tanzania imejaaliwa wachezaji wenye vipaji vya mpira lakini huwezi kuwa mchezaji mzuri kama haupati nafasi ya kucheza kwenye timu yako lazima kiwango chako kitaporomoka.

“Namshauri atafute changamoto mpya nje ya Simba ili aimarishe kiwango chake kuliko kuendelea kung’ang’ania kwenye timu ambayo hana nafasi ya kucheza.”

STORI: WILBERT MOLANDI NA HUSSEIN MSOLEKA

Toa comment