The House of Favourite Newspapers

Saidi Ntibazokiza ‘Saido’ Amuwekea Mtego Mayele Ligi Kuu

0
Mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Saidi Ntibazokiza ‘Saido’.

KIUNGO Mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Saidi Ntibazokiza ‘Saido’ amesema hafikirii Tuzo ya Ufungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu, bali kitu chake muhimu ni kuipa matokeo mazuri timu yake.

Kauli hiyo huenda ikawa mtego kwa mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani, Fiston Mayele ambaye yupo katika mbio za ufungaji bora katika msimu huu.

Mayele mwenye mabao 16 katika Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa kinara, amemzidi Saido bao moja, huku zikibaki mechi mojamoja kwao kukamilisha msimu huu.

Akizungumza na Spoti Xtra, Saido alisema akili yake ipo katika kuipa matokeo mazuri Simba, na sio kufikiria Tuzo ya Ufungaji Bora.

Saido alisema kwake atahakikisha anawatengenezea wenzake nafasi za kufunga na ikitokea akapata upenyo wa kufunga, basi ataitumia vema kwa kupachika bao.

Mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani, Fiston Mayele.

Aliongeza kuwa, ikitokea akawa mfungaji bora msimu huu, atafurahia licha ya kutokuwepo katika malengo yake.

“Mimi akili yangu inafikiria katika kuisaidia timu ili ipate matokeo mazuri ya ushindi katika michezo hii ya mwisho.

“Hivyo nitawatengezea wachezaji wenzangu nafasi za kufunga na kama ikitokea nikapata na mimi, basi nitaitumia vema kufunga.

“Naheshimu ubora na uwezo wa Mayele katika ufungaji, lipo wazi yeye ni mshambuliaji bora mwenye kiwango kizuri ndani ya misimu hii miwili ambayo amejiunga na Yanga,” alisema Saido.

Rekodi zinaonesha kwamba, Mayele akiwa na mabao 16, ana pasi tatu za mabao, huku Saido mwenye mabao 15, ana pasi 12 za mabao.

Saido katika mchezo wa juzi Jumanne dhidi ya Polisi Tanzania, alifunga mabao matano.

Akiwa ndani ya Simba aliyojiunga nayo dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Geita Gold, Saido ameandika rekodi ya kufunga hat trick mbili dhidi ya Tanzania Prisons na Polisi Tanzania, huku Mayele akiwa na hat trick moja aliyoipata mbele ya Singida Big Stars.

Ikumbukwe kwamba, Saido amecheza mechi 22 za ligi msimu huu na kuhusika kwenye mabao 27, wakati Mayele akiwa amecheza mechi 25, amehusika kwenye mabao 19.

STORI NA WILBERT MOLANDI NA LUNYAMADZO MLYUKA

MAMA BONGE AANIKA UKWELI KUUZA NYUMBA AMTOE MBOWE GEREZANI, AONESHA KADI ZA CHAMA-“CCM KINDAKINDAKI”

Leave A Reply