The House of Favourite Newspapers

Sajent usitukane mamba wakati hujavuka mto

0

Sajent-1.jpgMsanii wa sinema za Kibongo, Husna Idd ‘Sajent’.

KWAKO msanii wa sinema ambaye bado unaendelea kufurukuta ili uweze kutoboa katika anga la sinema za Kibongo, Husna Idd ‘Sajent’, mambo vipi? Uko poa, pole kwa mihangaiko ya kila siku ya kujitafutia riziki.

Ukitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima. Namshukuru Mungu, naendelea na shughuli zangu za kila siku. Tunaendelea kuwahabarisha, kuwaburudisha Watanzania kupitia magazeti Pendwa ambayo yanaongoza kwa kusomwa nchini.

Baada ya salamu hizo, moja kwa moja niende kwenye dhumuni la barua hii. Nimekuandikia barua hii ili kutaka kukukumbusha kwamba umepitiwa. Kitendo cha kuwatukana waandishi wa habari mtandaoni, tena wa Global Publishers, hakikuwa cha kiungwana hata kidogo.

Ulikosea maana najua unajua umuhimu wa vyombo vya habari lakini kama umejisahau, nitakukumbusha kwa barua hii. Vyombo vya habari ndivyo vinavyotangaza kazi zenu. Waandishi wa habari hususan wa Global ambao ‘wanadili’ zaidi na habari za burudani na sanaa kwa jumla ndiyo ‘silaha’ muhimu katika kazi zako.

Ndiyo ambao wanaweza kusafirisha habari zenu hadi kwa wananchi kuweza kujua mnafanya nini kila uchwao. Kujua una mipango gani katika sanaa, kutangaza kazi mpya na mambo mengine mengi ambayo yanafanana na hayo.

Wewe ni shahidi. Wakati tunaanza kukuandika katika Shindano la Kimwana Manywele, hakuna ambaye alikuwa anakujua mjini. Baada ya kuibuka kidedea katika mashindano hayo, ushukuru Mungu maana tuliendelea kukusapoti na ukaendelea kuzungumzwa na Watanzania.

Hata ulipoanza kufanya uigizaji, ni magazeti ya Global pekee ambayo yalikupa nafasi kubwa ya kuweza kujitangaza. Angalau nyota yako ikaanza kung’aa, ukapata hata bahati ya kuandikwa uhusiano wako wa kimapenzi na staa aliyekuwa na jina kubwa kimuziki, Charles Gabriel Mbwana ‘Chaz Baba’.

Urafiki wenu ukatengeneza kapo ya watu maarufu kupitia magazeti ya Global na wewe ukawa juu. Hata mlipokuja kuachana akiwa tayari ameshazaa mtoto na wewe, Global haikuwa nyuma. Iliendelea kukumulika kila hatua.

Unaanzaje sasa kuwatukana waandishi? Ulilewa siku hiyo? Ulipitiwa? Unajiona umefika au ni shetani alikupitia? Mbona bado una safari ndefu kisanaa! Au na wewe unajiona tayari umeshafikia malengo yako ya kuwa staa? Huhitaji kukua zaidi ya hapo?

Kama ni kweli unahitaji kusonga mbele, inakupasa ukiri kwamba umekosea na uombe radhi. Kutukana ni hulka, ukiendelea nayo utawatukana wengine na wengine ambao utakuwa unahitaji msaada wao. Jirekebishe maana tabia ya kutukanatukana si nzuri.

Hata kama mtu amekukwaza kwa namna moja au nyingine, tumia busara katika kufikisha hisia zako. Kama uliona hao waandishi hawakutenda haki katika habari, kuna viongozi wao. Ungefika ofisini na kuzungumza nao  wangelifanyia kazi katika ngazi ya uongozi, lingeisha kiofisi na si kukimbilia mtandaoni.

Nimalizie kwa kukwambia hujavuka mto, usitukane mamba. Kama ni muungwana na unahitaji sanaa kuendesha maisha yako, omba radhi na maisha yaendelee.

Mimi ni kaka’ko

Erick Evarist

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS

GLOBALBREAKINGNEWS100.jpg

Leave A Reply