The House of Favourite Newspapers

SAKATA LA CAG: POLEPOLE AONYESHA SH. TRILIONI 1.5 ZILIPO

 

KATIBU wa Itikadi na uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amewashutumu baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambao wamekuwa wakipotosha ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na akasema inafaa pawekwe utaratibu ili  waanze kuchukuliwa hatua za kisheria.

 

Aidha, Polepole ameipongeza serikali ya CCM chini ya Rais Magufuli kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuanika hadharani ripoti ya CAG na kuchukua hatua kwa wanaofanya ubadhirifu unaobainishwa. Amesema pia vipo vyama vya siasa vinatumia fedha ya umma na havitoi hesabu.

 

“Vipo vyama vimetumia zaidi ya Sh. Milioni 700 bila kutoa hesabu, pia vipo vyama ambavyo vinatumia fedha bila kufuata kanuni za kihasibu. Kuna chama kinaitwa ABC, SAU, CHADEMA, wametumia fedha bila kutoa hesabu zilivyotumika na pia kutumia fedha zaidi ya bilioni 2.2 bila kupeleka benki, hawa wanawezaje kuikosoa serikali?

 

“CHADEMA imefanya manunuzi ya zaidi ya shilingi bilioni 24 bila kushindanisha, wakati ndiyo hao wanaoisema serikali. Inapotoshwa kuwa CCM imekopa ndani ya mifuko ya hifadhi ya jamii, CCM ina utaratibu wake wa ndani wa kulinda maslahi ya watumishi wake tofauti na vyama vingine.

 

“Zitto Kabwe ndiye anaongoza kupotosha ripoti ya CAG kwa kukurupuka na ripoti asizozielewa, na kusema taarifa ya CAG ilikuwa imeshapitiwa na wao kwanza. Anasema Sh. Trilioni 1.5 zimepotea, na kufafanua kuwa sasa kuna mtindo mpya ambao unafuata vigezo vya kimataifa vya ukaguzi wa hesabu za umma,” amesema Polepole.

 

Polepole amefafanua kwamba Serikali imekusanya trilioni 25.3, na kusema ili kujua makusanyo halisi unachukua Sh. trilioni 25.3, unatoa makusanyo tarajiwa (receivables Sh. bilioni 687.3), pia unatoa Sh. bilioni 203.92 ambazo ni fedha zilizokusanywa kwa ajili ya Zanzibar, ambazo haisomwi kwenye Bajeti ya Serikali ya Muungano, utapata Sh. trilioni 24.4 ambazo ndiyo makusanyo halisi ya mwaka 2017/208.

 

“Zitto anadai pesa zilizotumika kutoka trilioni 25.3 ni trilioni 23.79, hii kipindi mkaguzi anapita zilikuwepo fedha za serikali ambazo zilikuwa kwenye hatifungani (zilikuwa hazijaiva) ambayo ni shilingi 697.85 bilioni

 

“Ukichukua 697.85 bilioni ukijumlisha trilioni 23.5 unapata trilioni 24.4, na ukichukua 25.3 ukatoa 23.79 unapata 1.5 trilioni ambayo ndiyo Zitto anadai imeibiwa. Zitto hajui hesabu na anapaswa kumtafuta mwalimu,” alisema Polepole.

 

Ameongeza kwamba Zitto amepotosha kuhusu bilioni 219 ambayo ililipa madeni ya zamani ambayo hayakuwa yamepitishwa na Bunge huku akieleza kwamba hesabu za serikali zinawekwa kwenye vifungu, na kulikuwa na madeni mbalimbali yanayofikia bilioni 969 ambayo yalipitishwa na Bunge na serikali inayalipa baada ya kuyahakiki, hivyo bilioni 219 ni sehemu ya bilioni hizo 969 zinazofahamika na Bunge.

 

Katibu huyo alisisitiza kwamba Zitto amepotosha pia kuhusu serikali kukopa bilioni 500 ambazo ni zaidi ya ukomo iliyowekewa, huku akidai akisema jambo hilo analiachia Bunge na kutaka Zitto achukuliwe hatua kwa kupotosha. Amemwambia Zitto Kabwe mwaka 2020 atafute kazi nyingine kwa sababu watu wa jimbo lake wamechoshwa na siasa za barabarani lakini mambo ya msingi hayupo.

Comments are closed.