SAKATA LA DINI YA WANAYE… ZARI KAYAIBUA YALIYOLALA

DAR ES SALAAM: Ukifanya jambo na kulisahau usifikiri watu wote wasahaulifu kama wewe; kuna wakati watakukumbusha!  

 

Zarinah Hassan ‘Zari’ hivi karibuni ameibua yaliyolala baada ya kuposti picha akiwa na mwanaye Latifa Nasibu ‘Tiffah’ wote wakiwa wamevaa hijabu, vazi linalovaliwa sana na waislam huku pia akiposti picha ya ustadhi akisoma Quran.

 

Wenye kumbukumbu zao baada ya kuona picha hizo, walimkumbusha kuwa mwaka jana alionekana akiwa kanisani na watoto wake wawili Tiffah na Nillan, jambo lililowaaminisha kwamba, wametulia kwenye ukristo mazima. “Dada mbona hueleweki, mara kanisani mara kwenye uislam, tushike lipi?” mtu mmoja aliposti komenti yake kwenye picha ya hijab aliyotupia Zari kwenye mtandao wa Instagram.

Hata hivyo, komenti za aina hiyo zilionekana kwa baadhi ya wafuasi wa Zari kama ni mashambulizi yasiyokuwa na sababu kwa mwanadada huyo aliyezaa watoto hao wawili na msanii nguli Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz.’

 

“Mwaka jana alipowapeleka kanisani watoto mlikuja juu kwamba hao ni watoto waislam, leo wameletewa shehe awape baraka bado mnalalamika, litendwe lipi mridhike nyie?” Posti nyingine ilisomeka.

Katika tukio la mwaka jana kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na Zari, hakuwapeleka watoto kanisani kuwabadili dini bali alihudhuria nao ibada ya maombi, jambo ambalo si vibaya kwa sababu hata Wakristo wanaruhusiwa kushiriki maombi ya Kiislam.

 

Zari alikuwa na uhusiano ‘hoti’ wa kimapenzi na Diamond kiasi cha kubahatika kuzaa watoto hao, ingawa baadaye wawili hao waliachana na kila mtu kushika ‘hamsini’ zake. Zari kwa sasa anaishi na watoto wake nchini Afrika Kusini ambapo Diamond amebaki na maisha yake ya Kibongo.

Mara kadhaa Diamond na Zari wamekuwa wakitakiwa na mashabiki wao kuufufua uhusiano wao ikiwezekana kufunga ndoa ya kiislam kwa imani kwamba ‘kapo’ yao ilikuwa ikiwavutia wengi. Ingawa Diamond amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanadada mwingine kutoka Kenya Tanasha Donna, bado penzi hilo jipya limeshindwa kufukia nyayo za uhusiano wake na Zari.

Stori: Mwandishi Wetu, Amani

Toa comment