The House of Favourite Newspapers

Sakata la Gari Jipya, Mobeto, Mama’ke Wajichanganya

0

LILE sakata lililochukua nafasi kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii hasa Instagram la mwanamitindo maarufu, Hamisa Mobeto kudaiwa kudanganya kuwa amejizawadia gari katika bethidei yake, limeibua sintofahamu kutokana na mama na mwana kutofautiana.

 

Mkanganyiko huo ulikuja baada ya Mobeto kudai kuwa amejizawadia gari aina ya Toyota Range Rover ambapo wafukunyuzi wa mambo walisema kuwa mwanamitindo huyo kadanganya kwani ni gari la mtu aliyejulikana kwa jina la Juma na siyo lake.

 

Kutokana na sakata hilo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta mama wa Mobeto, Shufaa Rutiginga kupitia kwa meneja wa mwanaye huyo ambapo alitoa kauli inayoenda kinyume na ile ya mwanaye huyo.

 

“Hilo gari ni la Mobeto na amepewa siku ya bethidei yake. Siwezi kusema amepewa na nani, wanaosema siyo lake watajua tu hakuna habari nyingine zaidi ya hiyo.

 

“Sijui ni lini watu watamuacha mwanangu maana kila atakachofanya wanamuweka kwenye mitandao! Sasa siwezi kuzungumza sana, kama gari siyo lake nawaachia wanaojua zaidi,” alisema mama Mobeto.

 

WATOFAUTIANA

Wakati mama anatoa kauli yake hiyo, kwa Mobeto ilikuwa tofauti kwani awali alisema amejizawadia mwenyewe, hivyo kuzua maswali zaidi kwa mashabiki.

 

CHANZO CHAANIKA MAPYA

“Gari ambalo Mobeto alisema amejizawadia kwenye bethidei yake ni geresha maana lina mwenyewe kwa sababu alipomaliza tu sherehe, lilirudishwa nyumbani kwa mwenyewe likiwa na mapambo yake kama lilivyoletwa kwenye ukumbi,” kilieleza chanzo ambacho kiko karibu na Mobeto.

 

Chanzo hicho kilizidi kuzungumza kuwa mwanaume huyo ambaye yuko karibu na msanii Mwijaku, mara nyingi walionekana pamoja wakiwa na gari hilo huku ikidaiwa msanii huyo ndio kacheza mchezo mzima.

 

“Mwijaku anajua kila kitu maana alisema kuwa gari hilo limetumwa kutoka Afrika Kusini wakati tangu mwezi wa tisa walionekana wakilitumia,” kilisema chanzo.

 

Alipotafutwa Mwijaku kwa ajili ya kujibu kuhusu mara nyingi kuonekana kuchonga mchongo mzima kuhusiana na gari hilo, alisisitiza kuwa gari hilo ni la Hamisa.

 

“Watu waache majungu kuhusu gari la Hamisa, watu walitaka nini ili waamini kwamba kweli ni lake amejizawadia,” alisema Mwijaku.

IMELDA MTEMA NA NEEMA ADRIAN

Leave A Reply