The House of Favourite Newspapers

Sakata la Madawa ya Kulevya Lachukua Sura Mpya

DAR ES SALAAM: Kufuatia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Februari 2, 2017 kutaja majina ya askari, watu wa kawaida na wasanii wakiwemo Wema Sepetu, Khalid Mohammed ‘TID’, Hamidu Chambuso ‘Nyandu Toz’, Herry Sameer ‘Blue’, Winfrida Josephat ‘Recho’, Rashid Makwiro ‘Chid Benz’ na Babuu wa Kitaa, wakihusishwa na matumizi na biashara ya madawa ya kulevya, Jeshi la Polisi limetangaza kuwasimamisha kazi baadhi ya askari wake waliotajwa kwenye sakata hilo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Ernest Mangu

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 4, 2017 kwenye Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, yaliyopo Wizara ya Mambo ya Ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Ernest Mangu amesema licha ya kusimamishwa kazi kwa askari hao ili kupisha uchunguzi dhidi yao, bado jeshi lake linaendelea na hatua nyingine ya kuwachunguza watu wengine wote waliotajwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekutwa na hatia.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na wanahabari.

Askari waliosimamishwa kwa tuhuma hizo ni SACP Christopher Fuime, Inspekta Jacob Swai, Sajenti Steven Ndasha, Sajenti Steven Shaga, Sajenti Mohamed Haima, Koplo Dotto Mwandambo, Koplo Tausen Mwambalangani, Koplo Benatus Luhaza, Koplo James Salala, Koplo Noel Mwalukuta, D/C Gloria Massawe na D/C Fadhili Mazengo.

Inspekta Jenerali Mangu, aliongeza kuwa wakati uchunguzi ukiendelea, Watanzania wanapaswa kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kutoa taarifa zote za uhalifu, ili kuhakikisha nchi inabaki salama.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.

Ilipofika muda wa maswali, waandishi wa habari walimuuliza Inspekta Jenerali Mangu kuhusu hatma ya wasanii waliokuwa wakishikiliwa kituo kikuu baada ya kujisalimisha kwenda kuhojiwa ambapo alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu kuna utaratibu maalum wa kulizungumzia.

Februari 2, mwaka huu, Makonda aliwataja mbele ya waandishi wa habari, askari, raia wa kawaida na wasanii waliokuwa wakituhumiwa kujihusisha na biashara au matumizi ya madawa ya kulevya, jambo lililowaacha watu wengi midomo wazi, hasa kutokana na watu maarufu na askari kujumuishwa kwenye kundi hilo, akiwataka wote waliotajwa, kwenda kujisalimisha wenyewe kwenye Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.

Siku moja baada ya Makonda kutoa tamko hilo, wasanii wanne, wakiwemo Wema Sepetu, TID, Nyandu Toz na Babuu wa Kitaa ambaye pia ni mtangazaji wa runinga, walijisalimisha kituoni hapo, kutii agizo la mkuu wa mkoa.

Wasanii hao walikutana na kundi kubwa la watu nje ya kituo hicho, waliokuwa na shauku ya kuwaona wakijisalimisha ambapo mahojiano yalianza kwa msanii mmoja baada ya mwingine, sambamba na askari kadhaa.

Baada ya mkutano wa Inspekta Jenerali Mangu na waandishi wa habari, waandishi wa mtandao huu walikwenda mpaka Kituo Kikuu cha Polisi ili kujua hatima ya wasanii waliokuwa wakishikiliwa.

Baada ya kufika kituoni hapo, waandishi wetu walipata fursa ya kuzungumza na Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, ambapo alisema:

“Tumewahoji lakini siwezi kusema kama tumewaachia au bado tunawashikilia kwa sababu kuna utaratibu wake wa kutoa taarifa hizo. Jumatatu kutakuwa na mkutano wa waandishi wa habari na tutawaeleza.”

Save

Comments are closed.