The House of Favourite Newspapers

Sakata la Mirathi ya Marehemu Mpakanjia kwa Wanaye Lamalizwa Mahakamani

0
Marehemu Mpakanjia enzi za uhai wake alizaa na marehemu Amina Chifupa mtoto aitwaye Abdulrahman.

 

Sakata la utata wa mgawanyo wa mali zilizoachwa na aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa nchini, Mohamed ‘Meddy’ Mpakanjia lililozua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii miezi kadhaa iliyopita, limemalizwa katika Mahakama ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

 

Watoto watatu wa marehemu, akiwemo aliyezaa na marehemu Amina Chifupa, Abdulrahman Mpakanjia, wamekubali kupokea mgawanyo wa mali zilizoachwa na marehemu baba yao, baada ya awali kugomea mchakato huo wakidai wamedhulumiwa na msimamizi wa mirathi.

 

Baada ya suala hilo kufikishwa mahakamani, imebainika kwamba si kweli kwamba walikuwa wamedhulumiwa na msimamizi huyo wa mirathi kama walivyodai awali ambapo watoto hao wa marehemu wamekubaliana na maelezo yaliyotolewa mahakamani kuhusu thamani halisi ya mali zote zilizoachwa na marehemu baba yao na kumuomba radhi msimamizi huyo wa mirathi kwa tuhuma walizomtolea awali.

 

Akizungumza na mwandishi wetu, kaka wa marehemu Mpakanjia, Abdul Mpakanjia amesema watoto wote wa marehemu wameridhishwa na uamuzi wa mahakama na kukubali kukabidhiwa urithi wao ambapo utekelezaji wa suala hilo umeanza na unaendelea kutoka kwa msimamizi wa mirathi.

 

“Tatizo lililokuwepo ni kwamba kulikuwa na sintofahamu kuhusu kiwango halisi kilichoachwa na marehemu, watoto wake walikuwa wakilalamika kwamba wanahisi wamedhulumiwa na msimamizi wa mirathi lakini baada ya mahesabu kufanyika mbele ya wanasheria, watoto na ndugu wote wameridhia mgawanyo huo kwa hiyo kinachofuatia kwa sasa ni utekelezaji wa mgawanyo ambao tayari umeanza,” alisema.

 

Akaongeza kuwa mali alizoacha marehemu ni pamoja na fedha taslimu ambazo tayari zimegawanywa sawa kwa watoto wote watatu, nyumba tatu zilizopo maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, kampuni tano pamoja na gereji ya magari iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.

 

Mwandishi wetu amemtafuta Abdulrahman Mpakanjia ambaye kama ilivyoelezwa ni mtoto wa marehemu Amina Chifupa, ambapo amekiri kumalizika kwa mgogoro uliokuwepo mahakamani na kueleza kuwa kinachosubiriwa kwa sasa ni kutekelezwa kwa maamuzi ya mahakama.

 

“Tunamshukuru Mungu suala limeisha vizuri kabisa, sisi watoto wote tumekubaliana na mahesabu yaliyowasilishwa mahakamani na tayari mgawanyo wa baadhi ya vitu umeshaanza na naamini utaisha salama ili kila mmoja aweze kunufaika kwa kile alichotuachia marehemu baba,” alisema Abdulrahman.

Leave A Reply