The House of Favourite Newspapers

Sakata la Wanawake Kutelekezwa Kimewaka!

 

SALAAM: Kimewaka! Ndivyo unavyoweza kusema! Siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda kutangaza ‘operesheni’ ya kusaidia wanawake waliotelekezwa ofisini kwake, mapya kibao yamebumburuka ambapo muigizaji Blandina Chagula ‘Johari’ na Shamsa Ford nao wameliamsha dude kwa Makonda.

 

Kama hiyo haitoshi, jamaa mmoja aliyefahamika kwa jina la Ramadhani Ibrahimu, mkazi wa jijini hapa ambaye anafanyia kazi zake Dubai, anadaiwa kumtwanga mkewe talaka kisa kikiwa ni kumbambikia ujauzito.

 

TWENZETU KWANZA MITAANI

Mara baada ya mamia ya wanawake kujitokeza ofisini kwa Makonda, Ilala jijini Dar kwa takriban wiki nzima, mtaani kumedaiwa kulipuka matukio tofautitofauti, kuna ambao wamedaiwa kupewa talaka na waume zao baada ya kuonekana kwa Makonda na wengine kuchezea kichapo ama kumwagwa mazima.

 

“Yani hili suala la Makonda limezua balaa, huku mtaani kwetu Kigogo ni vurugu, kuna jamaa kamtandika makonde mwanamke wake baada ya kuona ameenda kwa Makonda lakini kuna mwingine kamtwanga talaka baada ya kuona mkewe kwenye luninga,” alisema Abdul Kaisho, aliyepiga simu chumba cha habari.

 

WANAUME, WANAWAKE VURUGU

Mbali na tukio hilo, simu mbalimbali zilizopigwa chumba cha habari, zilieleza namna ambavyo suala hilo la Makonda lilivyozua tafrani mitaani.Yaani watu hatumwi maji  Wanaume wana hofu ya kutajwa, lakini hata wanawake nao waliowakimbia wanaume nao wanaishi kwa hofu baada ya Makonda kuwataka nao wakalalamike.

 

“Yani vurugu mtindo mmoja, wanaume wanawachimba mikwara wanawake zao wasiende lakini wanawake nao wanagoma, wanasema lazima waende hata kama siku zimepita,” alisema Dullah, aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa Tandale-Uzuri, Dar.

 

TURUDI SASA KWA MBONGO AISHIE DUBAI

Wakati sakata la Makonda likizidi kutimua vumbi, taarifa mpya iliibuka kwamba, Ramadhani Ibrahimu, mkazi wa Kinondoni jijini Dar, naye ametangaza kumpa talaka mkewe kwa madai ya kubeba ujauzito ambao si wake. Kwa mujibu wa chanzo ambacho kipo karibu na familia hiyo, tangu ujauzito wa mwanamke huyo uwe mkubwa katika familia yake pamekuwa hapatoshi kwani mwanaume huyo anadai ujauzito siyo wake.

 

“Yaani kwenye ndoa hizi kuna mambo. Hawa watu mimi ninawafahamu vizuri, sasa tangu mke wa Ibra apate ujauzito, mambo yamekuwa si mambo na hivi karibuni jamaa ameamua kumtwanga mkewe talaka. “Mimi ninaweza kuwasaidia mkampata huyo mwanaume na akaweza kuwaeleza kila kitu kilichotokea kwenye familia hii,” kilidai chanzo hicho.

 

 

RISASI LIVE NA IBRA

Baada ya Risasi kukisikiliza chanzo hicho, liliweza kuomba mawasiliano ya jamaa huyo ambaye yupo nje ya nchi huko Dubai na kumuuliza ukweli wa madai hayo.Alipopatikana, Ibra alidai kubambiwa ujauzito na kudai kuwa kwenye ndoa yake kulikuwa na misukosuko iliyosababisha ammwage mkewe.

 

“Unajua mimi na mke wangu tunaishi mbali kwa muda mrefu. Mimi nakaa Dubai na mke wangu anakaa Dar na nimemuoa kwa ndoa kabisa.“Sasa kwa mara ya mwisho nimekutana naye miezi mitano iliyopita, lakini cha kushangaza hivi karibuni nimegundua ana ujauzito wa miezi nane.

 

“Kiukweli suala hilo lilinisikitisha mno, lakini mbali na hilo kulikuwa pia na mambo mengine yanaendelea ambayo kwa muda mrefu nilikuwa ninayavumilia lakini imetosha,” alisema Ibrahimu. Risasi ilimuomba Ibra kuthibitisha juu ya maneno yake, ambapo aliweza kutuma picha akiwa na mkewe, mawasiliano pamoja na nakala ya talaka.

 

TWENZETU KINONDONI

Baada ya kutumiwa mawasiliano na maelekezo ya kumfikia mwanamke, Risasi lilifunga safari mpaka nyumbani kwao na mwanamke maeneo ya Kinondoni Stereo, ambapo mwanamke huyo hakuweza kupatikana zaidi alipatikana mmama mmoja aliyejitambulisha kama mama wa mke wa Ibra.

 

“Ni kweli ninamfahamu huyo mwaname (Ibra), alikuwa mume wa binti yangu lakini amekwishampa talaka sasa anamfuatilia wa nini?“Kama amempa talaka basi aachane naye, sasa anawezaje kuwa na mwanamke ambaye haelewani na wakwe zake!”Alisema mama huyo (jina tunalihifadhi kwa sababu maalum za kimaadili) na baadaye kukataa kuendelea kuhojiwa na waandishi.

 

JOHARI NA SHAMSA SASA

Wakati wanawake kibao wakimiminika kwa Makonda, wasanii wa filamu Bongo, Shamsa Ford (pichani) na Blandina Chagula ‘Johari’ nao wamesema wakati wowote (kuanzia juzi Alhamis) wanaliamsha dude ofisini kwa Makonda kwani nao wana malalamiko yao mazito ambayo wanaamini watasaidiwa.

STORI: BONIFACE NGUMIJE NA NEEMA ADRIAN, RISASI JUMAMOSI

LIVE: MAKONDA AFUNGUKA A-Z ALIYOJIONEA ZOEZI LA WANAWAKE WALIOTELEKEZWA

Comments are closed.