The House of Favourite Newspapers

Sakho Awekwa Chini ya Uangalizi Simba SC

0

HUKU wakijiandaa na mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, kiungo mshambuliaji wa Simba, Pape Ousmane Sakho amewekwa chini ya uangalizi maalum wa madaktari kufuatia majeraha aliyoyapata katika mchezo wao uliopita dhidi ya Dodoma Jiji.

 

Katika mchezo huo dhidi ya Dodoma, Simba walilazimika kufanya mabadiliko matatu ya lazima kutokana na majeruhi ambapo alianza kutoka Pape Ousmane Sakho dakika ya 12 ya mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Rally Bwalya, dakika ya 41 Kennedy Juma alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Henock Inonga Baka, kabla ya dakika ya 63 Taddeo Lwanga kutoka na kuingia Duncan Nyoni.

 

Kati ya nyota hao, tayari Lwanga na Kennedy wameshapona na kuanza mazoezi pamoja na nyota wengine waliokuwa na majeraha, huku Sakho pekee akisaliwa kuwa mchezaji pekee ambaye mpaka sasa anasubiri ripoti ya daktari.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mkuu wa Kitengo cha Maudhui wa Simba, Ally Shatry alisema: “Kikosi kinaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wetu ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana ambao kwetu utakuwa mchezo wa kwanza katika michuano ya msimu huu.

 

“Habari njema kwetu na kwa benchi la ufundi ni kuwa, tayari majeruhi wote wa kikosi wamepona na kuanza mazoezi, isipokuwa Pape Ousmane Sakho ambaye alipata majeraha katika mchezo wetu uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, kwa sasa amewekwa chini ya uangalizi maalum wa madaktari ili kujua kama atakuwa tayari kwa ajili ya mchezo huo.”

JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave A Reply