Saleh Jembe: Mnguto na Kasongo Wameondolewa Kwa Siasa

Katika kile kinachoonekana kuwa kipindi kigumu kwa uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Mwenyekiti wa Bodi hiyo Steven Mnguto kujiuzulu, huku Ofisa Mtendaji Mkuu, Almasi Kasongo, akisimamishwa kazi kwa maelekezo ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao mnamo Juni 13, 2025 imethibitisha kupokelewa kwa barua ya kujiuzulu ya Mnguto. Wakati huo huo, hatua ya kumsimamisha Kasongo imezua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa soka nchini.

Mabadiliko haya makubwa yamepokewa kwa mitazamo tofauti kwa baadhi ni ushindi, lakini kwa wengine ni dalili ya siasa kuingilia michezo.
Mwandishi mkongwe wa habari za michezo, Saleh Ally ‘Saleh Jembe’, hakusita kueleza maoni yake kwa kupitia mitandao ya kijamii:
“Steven Mnguto ameenda, Almasi Kasongo amesimamishwa na kwa wengi hii ni furaha kuu. Kosa lao? Hii itabadilisha nini katika soka letu? Kwa faida ya nani?”
Akiendelea kwa hisia nzito, Saleh alionya kuhusu matumizi ya nguvu na siasa ndani ya soka:
“Siasa ya soka imewaondoa lakini si mwisho kwao. Tukubali, hawana kosa wala hatia. Na kama tunaamini dhulma ni jambo sahihi, basi tukumbuke: Dhulma hurejea… NITAWAKUMBUSHA.”.