Samaki Amrukia Kutoka Majini, Amtoboa Shigo

KIJANA Muhammad Idul (16) Raia wa Indonesia ameelezea kisa alichokumbana nacho kwa mara ya kwanza wakati alipokuwa anaogelea na ghafla akaona samaki ametoka majini, akamrukia na kujikita shingoni mwake kwa kumdunga na sehemu zilizochongoka za mwili wake. (Tahadhari: Taarifa hii huenda ikawa na picha za kuwaogofya wasomaji).
Muhammad ameelezea vile samaki aina ya ngarara alivyoruka kutoka majini na kumdunga kwenye shingo yake, na kulazimika kuogelea kwa haraka kuelekea ufuoni kabla ya kukimbizwa hospitalini kwa dakika 90 garini.
Kwa kijana huyo wa miaka 16 kuwa hai, na kuweza kusimulia yaliyompata imekuwa kama muujiza baada madaktari kumfanyia upasuaji.
Alivyodungwa shingoni
Jeraha alilopata Muhammad limemfanya kuwa maarufu baada ya picha za samaki aliyemdunga shingoni kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuonekana kote ulimwenguni. Anasema walipanga kuvua samaki usiku akiwa pamoja na rafiki wake wa shuleni aitwaye Sardi.
“Mashua ya Sardi ilitangulia na mimi nikamfuata kwa kutumia mashua nyengine,” anakumbuka kilichotokea. “Takriban mita 500 kutoka ufuko wa bahari, Sardi akawasha taa. Samaka aina ya ngarara aliruka kutoka kwenye maji na kuniuma shingo yangu,” anasema.
Hapohapo, Muhammad alianguka kando ya mashua huku giza likiwa limetanda kila sehemu. Samaki huyo mrefu, mwembamba na mwenye taya kali akamuuma shingoni, chini ya kidevu hadi kwenye fuvu lake.
Hata baada ya kumdunga, samaki huyo alikuwa bado anamyumbisha kijana huyo majini wakati akijaribu kutoroka. Muhammad alimshika samaki huyo kwa nguvu akitumai kwamba hatafanya maafa zaidi katika jeraha alilopata.
“Nilimuomba Sardi usaidizi – na yeye akanishauri nisijaribu kumtoa samaki kwa sababu ningetoa damu nyingi,” amesema.
Hatimaye vijana hao walifanikiwa kuogelea hadi ufukoni huku Muhammad akiwa amemshikilia samaki huyo ambaye bado alikua amejikita pale alipomdunga shingoni.

Babake Muhammad aitway Saharuddin alimkimbiza hospitalini Bau-bau, karibia saa moja na nusu kutoka kijijini kwao kusini mwa Buton, eneo la kusini-mashariki mwa Sulawesi. Baada ya kufika hospitalini, madaktari walifanikiwa kukata mwili wa samaki lakini wakashindwa kutoa mdomo wake uliodunga shingoni kwa sababu ya ukosefu wa vifaa stahiki.
Hivyo basi wakahitajika kusafiri hadi hospitali ya mkoa iliyopo Makassar, mji wa kusini mwa Sulawesi. Katika hospitali kubwa ya Wahidin Sudirohusodo, wafanyakazi walishikwa na bumbuazi baada ya kumuona mwathirika.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Khali Saleh alisema kilikuwa ni kisa cha kwanza cha aina hiyo, na walihitaji wataalam watano ili kuondoa ka makini sehemu ya samaki aliyesalia shingoni mwa mwathirika, upasuaji uliochukua saa moja. Siku tano baadaye, Muhammad alifungwa bendeji na hakua tena na maumivu na ingawa hakuweza kugeuza shingo yake upande wa kulia lakini aliweza kutabasamu.
Hata hivyo, itamchukua muda kidogo ili kupona kabisa,
“Tunafuatilia hali yake. Huenda akatolewa hospitalini siku chache zijazo lakini hawezi kwenda kijijini ka sababu bado anahitaji kuonwa na madaktari,” Khalid Saleh ameelezea.
Aidha, licha ya tukio hilo, bado Muhammad ana ndoto ya kuendelea kuvua.
“Ninachohitaji kufanya ni kuwa mwangalifu zaidi wakati mwingine. Samaki aina ya ngarara hawawezi kuhimili mwangaza – na hiyo ndiyo sababu aliruka kutoka kwenye maji na kunidunga shingoni,” amesema.

