The House of Favourite Newspapers

SAMATTA, DIAMOND, MAJUTO NI DARASA TOSHA!

 HAKUNA mtu ambaye anakataa kwamba pesa sasa hivi imekuwa ngumu kupatikana. Bila kufanya kazi kwa juhudi na maarifa utaishia kusema, maisha ni magumu sana! Lakini wakati wewe ukisema hivyo, wapo ambao wanapiga pesa kupitia shughuli mbalimbali.

 

Kwa maana hiyo kumbe suluhisho la hali ngumu ni kufanya kazi kwa bidii. Lakini kupitia makala haya pia niwakumbushe kwamba, wakati tunahangaika kutafuta pesa, tutenge muda wa kufanya ibada. Tusijiweke bize kusaka pesa usiku na mchana na tukamsahau Mungu.

 

Tukumbuke kwamba, bila Mungu maisha yetu si lolote si chochote. Tutapata pesa lakini kwa kuwa hazina baraka ya Mungu, zitakwisha bila kufanyia mambo ya msingi na tutajikuta tumerudi kulekule kwenye umasikini.

Katika hilohilo la ibada, leo nataka kuwakumbusha jambo moja ambalo wengi wetu tumekuwa tukijisahau nalo sana. Nazungumzia kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu!

 

Kuna watu ambao Mungu amewajaalia kuwa na kipato kikubwa. Wamebarikiwa neema ya kuwa na pesa nyingi kuliko wenzao. Siyo kwamba wana akili sana au wanafanya kazi sana, hapana! Mungu tu kaamua kuwaruzuku lakini cha ajabu sasa, wamekuwa ni wagumu sana kurejesha shukurani kwa Mungu. Ni wagumu wa kutoa sadaka, kusaidia wasiojiweza.

 

Yaani wanajiangalia wao na familia zao tu. Mbaya zaidi hutawaona hata siku moja wakienda makanisani au misikitini kuabudu. Kwa kuwa wameshapata pesa, wanaona maisha wameyapatia. Huku ni kujisahau kubaya sana. Na niwaombee tu kwa Mungu wale ambao wamejisahau katika hili wazinduke, wakumbuke kwamba kuna kifo na Mungu atakwenda kuwauliza jinsi walivyoitumia neema aliyowapa.

 

Lakini nitumie fursa hii kuwatolea mfano baadhi ya mastaa ambao kiukweli wana kila sababu ya kuwa kioo kwa wengine ambao wamekuwa na mafanikio lakini hawawiwi kutoa kwa ajili ya Mungu.

 

Siku chache kabla ya mchekeshaji maarufu Bongo, Amri Athuman ‘King Majuto’ kufariki dunia, niliona moja ya mahojiano aliyoyafanya kwenye TV. Katika mahojiano hayo nilivutiwa sana na maelezo yake kwamba, kule kijijini kwake Tanga amejenga msikiti.

Alisema: “Najua siku moja nitakufa na Mungu ataniuliza nimetumia vipi neema aliyonijaalia. Ndiyo maana nikaamua kutumia sehemu ya kipato changu kujenga msikiti, namlipa imamu na gharama zote za kuuendesha ni juu yangu. Watu wanakuja tu kufanya ibada humu na mimi najisikia amani.”

 

Jaribu kuvuta picha; wakati mzee huyu anaongea maneno hayo, hakujua kwamba miezi kadhaa mbele atakufa na kuacha mali zake zote. Leo hii hayupo duniani, ameacha msikiti ambao kiimani tunaambiwa kila anayeingia kufanya ibada na yeye anapata thawabu. Mungu amjaalie kila la heri huko aliko.

 

Sasa najiuliza kwamba, ina maana bado hatuoni fundisho kupitia kile alichokifanya Mzee Majuto? Bado hatuoni umuhimu wa kutoa sehemu ya vipato vyetu kufanya yale ambayo yatatusaidia leo na kesho tukiwa tumeondoka duniani? Hata kama huwezi kujenga msikiti au kanisa peke yako, unashindwa hata kuchangia ujenzi wa kanisa au msikiti kwa kutoa shilingi 5000 au 10,000? Jibu unalo.

 

Lakini wakati ukiwa na maelezo hayo, ikukae kichwani pia kuwa kuna mastaa kama vile mwanasoka Mbwana Samatta ambaye anajenga msikiti mkubwa sana huko Vikindu, Pwani. Ni msikiti ambao mamilioni ya pesa yametumika mpaka sasa. Siyo kwamba hana mambo mengine ya kufanya, hapana! Amepata mafanikio makubwa kwenye soka, amekumbuka kwamba mafanikio aliyonayo bila Mungu asingeyapata.

 

Akaona cha kufanya ni kujenga nyumba ya ibada ambayo itamfanya Mungu azidi kumbariki katika maisha yake ya sasa na hata kesho ahera. Wewe unangoja nini? Ni kweli hujajifunza tu kupitia kwa mastaa hawa?

Najua kwamba wapo ambao wamefanya mambo makubwa kwa siri kwa ajili ya Mungu. Kama ni hivyo, Mungu azidi kuwabariki wafanye zaidi na zaidi. Lakini hata hawa ambao wamefanya na jamii imejua, siyo mbaya, naamini hawajajitangaza ili wasifiwe na watu bali wamefanya kwa ajili ya Mungu. Mungu azidi kuwabariki.

 

Ila sasa kwa alichokifanya Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliyejenga misikiti kule Morogoro na Mtwara, Mzee Majuto (Tanga) na Samatta (Pwani) iwe ni fundisho kwetu kwamba tunatakiwa kufanya mambo kwa ajili ya Mungu. Tutumie pesa zetu kufanya yale ambayo yatatunufaisha katika maisha yetu ya duniani na kesho ahera.

 

Hili siyo kwa mastaa tu, nimewatumia mastaa kwa kuwa wao ni kioo cha jamii lakini ishu ya kufanya mambo kwa ajili ya Mungu ni la kila binadamu.

Hii tabia ya mtu kujaaliwa pesa nyingi kisha zinaishia kwenye kufanya mambo ya anasa, niwaambie tu kwamba adhabu inaweza kuwa hapahapa duniani na hata baada ya kufa.

 

Ni wangapi unaowajua ambao walikuwa na uwezo mkubwa kipesa lakini leo hii wamerudi kwenye umasikini wa kutupwa? Unajua ni kwa nini? Ni Mungu kawaadhibu!

Usisubiri Mungu akuadhibu, tumia hata shilingi mia moja yako kufanya jambo lolote kwa ajili ya Mungu. Hiyo itakusaidia siku utakayoondoka katika mgongo wa ardhi.

Na Amran Kaima

Comments are closed.