Samatta kutupa karata ya pili Klabu Bingwa Ulaya leo

Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta, usiku wa leo akiwa na klabu yake ya KRC Genk anatarajiwa kushuka dimbani kwa mchezo wake wa pili wa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (Champions League) dhidi ya Napoli.

Genk, itakuwa nyumbani Ubelgiji katika dimba la Luminus Arena ikiwakaribisha miamba kutoka Italia klabu ya Napoli.

Katika mchezo wake wa kwanza Genk iliangushiwa kichapo kizito cha goli 6-2 ugenini dhidi ya RB Salzburg, huku Samatta akifunga goli moja la kufutia machozi. Katika mchezo huo, Samatta aliweka rekodi binafsi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Champions League na kufunga goli.

Napoli wao walianza kwa kuwafunga mabingwa watetezi Liverpool goli 2-0. Hivyo, Genk hii leo watakuwa tena na kibarua kizito cha kuwazuia Napoli. Hata hivyo, Genk haijawahi kupata ushindi hata mechi moja ya Champions League katika mara zote tatu walizoshiri michuano hiyo, kwani wamefungwa mechi moja tu nyumbani kati ya sita walizocheza na kutoka sare tano.

Napoli pia hawajapata ushindi wakiwa ugenini kwenye hatua ya makundi ya Champions League katika mechi sita zilizopita. Hivyo, japo si ya kutumainia, historia inaweza kuwabeba Genk na kupata walau sare. Mechi ya leo pia itawakutanisha tena Samatta na beki kisiki Kalidou Koulibaly raia wa Senegal.

Wawili hao waliminyana kwenye michuano ya Afcon Juni 23 mwaka huu ambapo Senegal ilipata ushindi wa 2-0 dhidi ya Tanzania. Je, Samatta ataweza kumpita Koulibally leo na kufunga goli baada ya kushindwa kufurukuta mbele yake Afcon?

Mechi hiyo itapigwa kuanzia saa mbili kasoro dakika tano za usiku kwa saa za Afrika Mashariki.


Loading...

Toa comment