The House of Favourite Newspapers

Samatta: Tutawachinjia mbali Malawi

0

IMG_6938

Mbwana Samatta.

Sweetbert Lukonge  na Hans Mloli
TIMU ya taifa, Taifa Stars, leo jioni itashuka uwanjani kupambana na Malawi katika mchezo wa awali wa kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2018 nchini Urusi.

Hata hivyo, nyota wa kutumainiwa wa Stars, Mbwana Samatta, amesema kuwa ana kazi kubwa ya kufanya katika mchezo huo kutokana na macho ya Watanzania wengi kuwa juu yake wakiamini kuwa ataiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi.

Hali hiyo inatokana na kiwango cha juu alichokionyesha hivi karibuni akiwa na klabu yake ya TP Mazembe, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Mereikh ya Sudan, alipoiwezesha timu yake hiyo kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu iliyopata kwenye mechi hiyo.

Akizungumza na Championi Jumatano, Samatta alisema kutokana na hali hiyo, atahakikisha anapambana vilivyo uwanjani ili Stars iweze kuibuka na ushindi.

“Naogopa sana kuzungumziwa kwa mabaya kila wakati kuwa sina msaada katika timu yangu ya taifa ila nikiwa na Mazembe nafanya vizuri, kusema kweli sipendi hilo linitokee kwa sababu hivi sasa Watanzania wengi macho yao yapo juu yangu.

“Hiyo inatokana na kazi kubwa niliyofanya hivi karibuni nikiwa na Mazembe baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo wetu wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Mereikh.
“Hivyo ili niweze kuilinda heshima yangu na imani waliyonayo dhidi yangu, nitahakikisha tunaibuka na ushindi,” alisema Samatta ambaye amejiunga na kikosi hicho juzi usiku.

Leave A Reply