The House of Favourite Newspapers

Samuel Sitta Umejibu Swali Langu!

0

sitta (1)Na Brighton Masalu

KITENDO cha aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta kutangaza nia ya kuwania tena kiti cha uspika katika bunge lijalo la 11, kimejibu swali langu la muda mrefu ambalo nimekuwa nikijiuliza kila wakati.

Swali kubwa lililokuwa likinitesa akilini mwangu, ni kitendo cha mwanasiasa huyo mkongwe nchini, kuamua kujenga hekalu la ofisini huko Urambo, jimbo alilokuwa akiliongoza wakati akiwa spika wa Bunge la Tisa.

 Sitta, ama kwa kiburi au ubabe wa asili, alilazimisha kujengwa kwa jengo hilo kwa gharama ya kutupwa kama ofisi ya spika!

Swali lililoibuka akilini mwangu, ni kwa nini Sitta aling’ang’ania kujenga ofisi hiyo jimboni kwake kwani yeye ni spika wa kudumu? Au Jimbo la Urambo Mashariki ndilo lina ‘waranti’ ya kutoa spika? Ni swali ambalo sikuwahi kupata jibu stahiki.

Mwaka 2010, Sitta aligombea tena uspika lakini akaangushwa na mwanamama aliyemaliza muda wake, Anne Makinda.

 Hata hivyo, kumbe hakukata tamaa kwani mapema baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Sitta ametangaza tena kukiwania kiti hicho kwa kujinasibu kuwa anazo sifa za kutosha kuliongoza bunge lijalo.

Sasa, angalau kwa mbali Sitta amenipa jibu la swali langu. Kumbe amejiandaa kuwa spika wa kudumu ndiyo maana alijenga ofisi kubwa kwa kodi za  wananachi jimboni kwake, akiwa na maana ya kuwa ataendelea kuwa spika kwa muda mrefu ujao.

Sitta, alijizolea umaarufu mkubwa akiwa spika wa Bunge la Tisa ambapo aliendesha vikao vya bunge bila upendeleo na kuruhusu mijadala hata ile ya hatari kwa serikali ijadiliwe huku akiwapa nafasi wabunge wa upinzani kuchangia hoja.

Ndiye aliyeruhusu mjadala mzito wa kashfa ya Richmond iliyosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa na ni Sitta huyohuyo kwa kutumia mamlaka aliyokuwa nayo alizima mjadala huo hali iliyompa umaarufu zaidi kama spika pekee aliyeongoza bunge kwa weledi mkubwa.

Kwa kutambua hilo, Sitta alifika mahali akajipambanua kama Mzee wa Kasi na Viwango.

Kuthibisha kuwa Sitta anaupenda uspika, katika Bunge Maalum la Katiba Mpya, alijitosa kuusaka uenyekiti na kufanikiwa kuupata ambapo aliliongoza bunge hilo.

Ahsante sana Samuel John Sitta kwa kujibu kwa vitendo swali langu, kumbe ulipokuwa unajenga ofisi ya spika huko Urambo ulimaanisha wewe ni spika wa kudumu katika nchi hii, nimekupata mzee wangu.

Hata hivyo, wengi wameendelea kuwa na maswali lukuki kwa nini Samuel Sitta anapenda sana kuwa spika? Wanasiasa wengi wa umri wake, tayari wamejiweka kando na mambo ya siasa lakini Sitta bado haoneshi hata dalili ya ‘kutundika daruga’ katika ulingo wa siasa.

Hawazii nafasi nyingine zaidi ya uspika, hajui na pengine ndiyo maoni yake, kwamba anaamini hakuna mwenye uwezo wa kukalia kiti hicho zaidi yake.

Samuel Sitta amejipambanua kweupe kuwa kwa muda mrefu amebaki na maumivu ya kukatwa mwaka 2010 kwa kile kilichoitwa “ni zamu ya mwanamke”.

Mbaya zaidi, Sitta anadaiwa kutangaza kwenda mahakamani endapo atafanyiwa tena zengwe katika nafasi hiyo.

Hapa napo nabaki na swali jingine, kwani ni lazima awe yeye tu kwenye nafasi hiyo ya uspika?

Hata hivyo, sijawahi kuwa na wasiwasi juu ya uwezo wa weledi wake juu ya uspika.

Anajua kulithibiti bunge, uwezo wake wa sheria umekuwa nguzo kuu kuwadhibiti wabunge hususan vijana katika uchangiaji hoja unaokiuka misingi na kanuni za bunge.

 Kila la heri katika mbio za kuusaka tena uspika ili uendelee kuitumia ofisi hiyo, ingawa kujitokeza kwako tena katika kinyang’anyiro hicho kunazidi kuibua maswali mengi zaidi.

Leave A Reply