Sanchi, Kiba Mambo ni Moto!

WAKATI wa Mungu kukujaalia mema ukifika, hakuna awezaye kuzuia! Ndivyo wanavyoamini baadhi ya wafuasi wa mwanamitindo maarufu Bongo, Janey Rimoy ambaye baada ya kubadili dini kutoka Ukristo na kuwa Muislam, sasa anaitwa Surraiya Rimoy ‘Sanchi’, Risasi Jumamosi linakupa ubuyu kamili.

 

SASA MAMBO NI MOTO

Kwa muda mrefu Sanchi alieleza ni kwa kiasi gani anamhusudu kimapenzi mfalme wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ bila mafanikio, lakini sasa inadaiwa wawili hao mambo ni moto!

 

NINI KIMETOKEA?

Mara tu baada ya Sanchi kutangaza kubadili dini na kuingia kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Kiba ambaye huwa hana utamaduni wa kuweka maoni yake kwenye picha au taarifa ya mtu katika Instagram, aliibuka na kumpongeza mrembo huyo, jambo ambalo limeibua gumzo kama lote.

 

Kiba ambaye ni Muislam na ‘hajamfolo’ mtu kwenye ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi milioni 5.3, alitupia ujumbe kwenye ukurasa huo wa Sanchi akionesha kufurahishwa na mwanamitindo huyo kuamua kubadili dini, jambo ambalo liliwashangaza wengi.

 

“Mmeona alichokifanya Kiba? Kiukweli si kawaida yake. Wewe tupe mfano, ni lini ulimuona Kiba ‘anakomenti’ kwenye picha ya mtu hapa Instagram?

“Hapa picha tumeshawekewa, cha msingi ni kuweka kichwa cha habari na kuandika caption..,” ilisomeka sehemu ya maoni mengi kwenye taarifa hiyo ya Sanchi kubadili dini.

 

HUYU HAPA SANCHI

Katikati ya mjadala huo mzito na kwamba ni muda mrefu sasa, Sanchi amekuwa akieleza namna anavyokunwa na Kiba, gazeti hili lilimtafuta mrembo huyo mwenye shepu matata ambaye kwa sasa yupo nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro na kumuuliza kuhusiana na pongezi hizo kutoka kwa Kiba.

 

Sanchi alisema kuwa, hata yeye aliona pongezi hizo za Kiba na kwamba, amefurahishwa mno kuona kuna watu wengi wamemuelewa alichofanya (kubadili dini).

“Nimeona, ameweka ujumbe kwenye picha niliyokuwa nimeposti na kueleza nimebadilisha dini.

 

“Unajua unapofanya kitu kizuri na mwenzako kukusapoti na kuona umefanya kitu kizuri, ni jambo jema sana,” alisema Sanchi ambaye ni miongoni mwa warembo maarufu kwenye mitandao ya kijamii (sosholaiti).

Alipoulizwa juu ya uhusiano wake na Kiba, alikiri kuvutiwa naye japokuwa hakutaka kuingia kiundani.

 

TUJIKUMBUSHE

Miaka mitatu iliyopita (2017), Sanchi alifanya mahojiano maalum (exclusive) na gazeti hili (yapo kwenye makabrasha yetu) ambapo alieleza ni kwa namna gani Kiba anamkosesha usingizi na kwamba ipo siku Mungu atajibu maombi yake.

 

Sanchi alisema kuwa, muonekano wa Kiba na sauti yake, ndivyo vitu ambavyo vimemchanganya kiasi ambacho anatamani aolewe naye.

“Yaani Kiba ananiua muonekano wake, sauti na vitu vingine kibao, natamani aniweke ndani kabisa.

 

“Hata kama watu watanishangaa kuhusu mimi kuwa mwanamke na kusema hili, lakini sitajali.

“Nasema hivi kuiridhisha nafsi yangu na wala si nafsi ya mtu mwingine, kama mtu ataona nimekosea, anaweza akakaa kimya tu.

“Aniache mimi na maamuzi yangu ya kusema maana kila mtu ana uhuru wa kuchagua kile anachojisikia,” alisema Sanchi ambaye ana Shahada ya Usimamizi wa Fedha kutoka Chuo cha IFM.

 

AAPA KUMNG’OA MTU

Wakati akifanya mahojiano hayo, Kiba wakati huo alikuwa na mtu wake, lakini Sanchi alisema hajali hilo.

Sanchi alikwenda mbele zaidi ambapo baada ya kuulizwa kuwa haogopi fujo kwani Kiba bado hajamwagana na huyo mtu wake wa wakati huo, mrembo huyo aliapa kufa naye mbele kwa mbele.

 

“Mimi nilikuwa najua wameshaachana na huyo mtu, lakini kama watakuwa wanaendelea, basi piga ua lazima nimtoe tu maana nimekamilika kila idara na mimi hisia zangu zipo kwake, kwa nini nijipunje?” alisema Sanchi.

 

AHADI YA KUBADILI DINI KISA KIBA

Kama hiyo haitoshi, mwanahabari wetu alijaribu kumbana Sanchi kuhusu suala la dini, kwani yeye ni Mkristo wakati Kiba ni Muislam, ambapo bila hiyana, mrembo huyo alisema yuko tayari kubadili dini bila shaka yoyote ile.

 

“Najua Kiba ni Muislam safi, lakini ikija kwenye upande wa dini wala hakuna taabu maana Waswahili wanasema kipendacho roho hula nyama mbichi, nitabadili tu, hakuna namna,” alisema Sanchi kipindi hicho, hivyo unaweza kujiongeza!

 

HAKUISHIA HAPO

Kama unadhani Sanchi aliishia hapo, unajidanganya kwa sababu mrembo huyo aliendelea kusema kuwa, kiu yake ni kuona suala hilo linatimia, atakachokifanya ni kuwa karibu na Kiba au marafiki zake ili iwe rahisi kufikisha ujumbe wake.

 

“Najua hata kupitia gazeti, anaweza kusoma na kujua kwamba ninampenda, lakini mimi kwa sasa nitakachokifanya nitajiweka karibu naye zaidi na ninaamini hakuna kinachoshindikana,” alisema Sanchi zamani hizo akijulikana zaidi kwa jina la utotoni la Sanchoka.

 

ALIPOTAFUTWA KIBA

Katika mahojiano hayo yaliyochapishwa na gazeti hili, alipotafutwa Kiba na kuelezwa hisia hizo za Sanchi, aliishia kucheka na kuuliza;

“Ni Sanchi yule maarufu kwenye mitandao?”

Alipojibiwa ndiyo, Kiba alikata simu bila kueleza kama atamkubalia ombi lake au la.

 

KIBA ANA MKE NA MTOTO

Hata hivyo, baadaye Kiba alifunga ndoa na mrembo kutoka Mombasa nchini Kenya, Amina Khaleef ambaye wamejaaliwa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Keyaan mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kadhaa.

STORI: IMELDA MTEMA, RISASI


Toa comment