The House of Favourite Newspapers

Sancho Anafikirisha

0

KATI ya wachezaji ambao mashabiki wa Manchester United walikuwa na imani naye kubwa msimu huu, ni winga Jadon Malik Sancho.

 

Raia huyu wa England mwenye umri wa miaka 21, kwa muda mrefu alikuwa akiwindwa na timu nyingi England zikiwemo Manchester City na Chelsea, lakini mwisho wa siku usajili uliopita akatua Man United.

 

Matarajio ya wengi ni kuona winga huyo akiendeleza makali yake kama alivyokuwa akifanya balaa ndani ya Ujerumani akiitumikia Borussia Dortmund.

 

Pale Dortmund, alikuwa akiiva sana na straika matata wa timu hiyo, Erling Halaand ambaye bado ameendelea kuwa moto licha ya Sancho kuondoka.

 

Hivi sasa Halaand anashirikiana vizuri na Jude Bellingham ambapo inaonesha wazi kuondoka kwa Sancho, kama hakuna kilichotokea. Wakati wenzake wakiendelea kung’ara, Sancho mambo yakemuwa magumu ndani ya kikosi cha Manchester United.

 

Winga huyo mpaka sasa akiwa amecheza jumla ya dakika 435, hajachangia upatikanaji wa bao lolote kati ya mabao 17 yaliyofungwa na Man United kwenye michuano yote msimu huu ndani ya mechi kumi.

 

Katika mechi hizo kumi, Sancho hakucheza mechi moja pekee ya Premier dhidi ya Aston Villa ambayo Man United ikiwa nyumbani ilipoteza kwa bao 1-0. Katika mchezo huo, Sancho aliishia benchi.

 

Kinachoonekana kwa winga huyu, mpaka sasa ameshindwa kumshawishi Kocha Ole Gunnar Solskjaer kumtia kwenye kikosi cha kwanza muda wote.

Hiyo inatokana na ushindani wa namba uliopo kikosini hapo na yeye kuonekana bado anahitaji muda zaidi kuimarisha kiwango chake.

 

Ukiangalia mechi tisa alizocheza Sancho tangu ajiunge na Man United, moja pekee dhidi ya West Ham United kwenye Kombe la Ligi ndiyo alicheza dakika zote tisini, lakini alishindwa kuisaidia timu yake kuepuka kichapo na kushuhudia wakitupwa nje ya michuano hiyo kwa kufungwa bao 1-0 wakiwa nyumbani.

 

Mechi alizoanza kikosi cha kwanza ni dhidi ya Villarreal na Young Boys zikiwa za Ligi ya Mabingwa Ulaya, mbili za Premier dhidi ya Wolves na Newcastle pamoja na ile ya Kombe la Ligi dhidi ya West Ham.

 

Mbaya zaidi ni kwamba, katika mechi hizo tano alizoanza kikosi cha kwanza, moja pekee alimaliza, huku ile dhidi ya Young Boys akitolewa mapema sana dakika ya 37 kufuatia Aaron Wan-Bissaka kuonyeshwa kadi nyekundu, Solskjaer akalazimika kumtoa Sancho na kumuingiza Diogo Dalot ili kuzuia mashambulizi langoni mwao. Haikusaidia, wakapoteza mchezo.

 

Wengi walitarajia kwamba kwa kuwa Sancho amerejea ardhi ya nyumbani basi atakuwa moto kushinda alivyokuwa ardhi ya ugenini kule Ujerumani.

 

Ndani ya Man United, Sancho anapata wakati mgumu zaidi kutoka kwa Mason Greenwood ambaye ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kucheza kwa nafasi hiyo kushinda wenzake.

 

Ukweli uliowazi ni kwamba, Greenwood amekuwa kwenye kiwango bora akifanikiwa kufunga mabao matatu katika mechi tisa ambazo ni sawa na zile alizocheza Sancho.

Greenwood alichomzidi Sancho ni mabao na muda wa kucheza pekee akicheza kwa dakika 724, ikiwa ni zaidi ya 289 ya zile za Sancho.

 

Ukiachana na Greenwood, Jesse Lingard na Anthony Martial, nao ni sehemu ya wachezaji wanaowania nafasi na Sancho. Katika eneo hilo, mchezaji inabidi ufanye kazi kisawasawa kuchukua namba moja kwa moja.

Leave A Reply