The House of Favourite Newspapers

`Sangoma’ anaswa na maini ya swala, ngozi ya simba

0

kamanda-KidavashariKamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari

MGANGA wa jadi na mkazi wa Sumbawanga mjini, mkoani Rukwa, Vitus Chomba (42), anashikiliwa na Polisi, wilayani Mlele, mkoani Katavi kwa tuhuma za kukutwa na nyara za Serikali bila kibali halali.

Ilidaiwa kuwa Choma amekuwa akitumia nyara hizo kupigia ramli chonganishi kwa jamii na kutibu wateja wake.

Nyara alizokamatwa nazo ni pamoja na nyama ya sungura pori, kwato za pundamilia, ngozi ya simba, maini ya swala na ngozi ya paka pori. Hata hivyo thamani ya vitu hivyo haikufahamika mara moja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alithibitisha kutokea kwa mkasa huo juzi saa moja jioni baada ya wakazi wa kijiji cha Inyonga, kata ya Nsekwa wilayani humo kumtilia shaka baada ya kukutana na wateja wake kwa siri kijijini humo wakati yeye ni mgeni katika eneo hilo .

Akizungumzia mkasa huo, Ofisa Mtendaji Kata ya Nsekwa, wilayani Mlele, Amos Ngozi, alisema alipokea taarifa kutoka kwa wakazi wa kata hiyo wakieleza kuna mtu anayekutana kwa siri kubwa na baadhi ya wakazi wa kata hiyo hali iliyosababisha hofu kwa baadhi kwa wananchi.

Alisema baada ya taarifa hizo alitoa taarifa Polisi ambapo kwa kushirikiana nao, walivamia nyumba anayoishi mganga huyo na kuifanyia upekuzi na katika begi lake la nguo walikuta ngozi ya simba, maini ya swala na ngozi ya paka pori.

Mtendaji huyo wa kata alisema vitu vingine walivyomkuta navyo ni nyama ya sungura pori, kwato za pundamilia na mkia wa nyati ambapo alieleza kuwa yeye ni mganga wa jadi na huwa anatumia vitu hivyo wakati wa kutibu ama kuroga kutokana na huduma anayohitaji mteja wake.

Alisema mganga huyo alifika katika kijiji cha Inyonga wilayani humo kwa lengo la kufuata wateja wake ambao walikuwa wamemwita awatibu na kudai alitumia vitu hivyo kuwatibia.

(PICHA ZOTE NA MAKTABA)

CREDIT: HABARI LEO

Leave A Reply