The House of Favourite Newspapers

SANGOMA MASHAROBARO WATIKISA

DAR ES SALAAM: VIJANA watano waliotajwa kuwa ni waganga wa kienyeji ‘sangoma’ tena masharobaro wameutikisa mji wa Morogoro baada ya kudaiwa kutoa mapembe (majini au uchawi) kwenye nyumba za watu, Amani lina habari nzima.  Mkazi mmoja wa Chamwino mkoani humo aliyejitaja kwa jina la mama Mwanaisha, aliliambia Amani kuwa, alikuwa amelala ndani, ghafla akasikia kelele nje, alipotoka akakutana na kundi la watu wakiwemo majirani zake; wakati akishangaa aliambiwa:

“Mama hapa nyumbani kwako kuna jini au kwa jina lingine pembe.” Wakati mama huyo akiendelea kutafakari kauli ya mmoja wa vijana hao masangoma, zogo la wananchi lilizidi na kumfanya awe na hofu. “Nikawauliza hilo pembe limetoka wapi maana mimi sijui hivyo vitu?” Mama Mwanaisha aliwauliza masangoma hao na kuongeza kuwa, hakujibiwa swali lake badala yake vijana hao waliendelea kumulikamulika eneo la nyumba yake kwa kutumia vioo wakiashiria kulitafuta lile waliloliita pembe mahali lilipokuwa limewekwa.

Amani lilipomuuliza mama huyo anadhani kwa nini masangoma hao na majirani zake walifika kwake kwa lengo hilo la imani za kishirikina? Alikana kujua chochote na kuongeza kuwa: “Nimeamka asubuhi nikawa napika vitumbua; kwa kuwa mimi ndiyo biashara yangu.

“Nikawa naendelea kuchoma na kuviuza, baadhi ya majirani zangu wakawa wanaulizana wanakuja saa ngapi (ina maana hao waganga) wakawa wanajijibu wenyewe, saa nne. “Mimi nikawa sielewi nini kinaendelea, baada ya kumaliza biashara yangu nikaingia ndani kulala. “Saa nane mchana ndiyo wakaja hao waganga, zogo lilipozidi pale kwangu polisi wakafika kuja kunisaidia kwa kuwakamata waganga hao.”

Amani lilipozungumza na mmoja wa majirani na mama Mwanaisha (jina linahifadhiwa) alisema, waganga hao walikuja Morogoro wakitokea mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kutoa uchawi kwenye nyumba za watu.

Waganga hao walisema yawezekana mtu asiwe mchawi lakini akawa ametupiwa jini na jirani yake; hivyo wao wana uwezo wa kuliona na kuliondoa hilo na uchawi wowote kwa kulipwa kiasi cha fedha.

“Niliingia tamaa ya kutoa hela shilingi elfu tano kwa sababu hao waganga walitoa pembe kwa jirani yangu (mwingine), nikasema yawezekana hata mimi imetupiwa jini nikaona niwape hiyo fedha ili walitoe,” alisema jirani huyo.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa, SACP Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa amewashikilia watuhumiwa hao kwa kufanya ramli chonganishi.

“Tunawashikilia watu watano ambao ni Idd Selemani Mpuye ‘Dk. Makata’, Athumani Mrisho Ramadhani ‘DK. Simba’, Chande Jumanne Rajabu ‘Dk. Simba Mtoto’, Mussa Kombo Ramadhani ‘Dk. Machinja’ na Seif Abdallah Lindoi ‘Dk. Kipara’,” alisema Kamanda Mtafungwa na kuwatahadharisha wananchi kuwa makini na watu hao.

Akaongeza kuwa uchunguzi unaendelea na kwamba ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Comments are closed.