Sarkodie mfalme wa Hip Hop Afrika
Mkali wa Hip Hop Ghana, Sarkodie.
Boniphace Ngumije
UWEZO ndiyo kigezo kikubwa kilichompa heshima Sarkodie kwenye medani ya muziki wa Hip Hop Afrika ambapo tofauti na kujinyakulia tuzo 42 na kuingia katika kinyang’anyiro mara 52, amekuwa akiandikwa katika chati mbalimbali za burudani zikiwemo MTV, The Guardian, BET na E-TV ya Ghana kuwa miongoni mwa wasanii watano wakali wenye heshima ya muda wote barani Afrika.
Katika ‘gamba’ lake la kusafiria anajulikana kama Michael Owusu Addo. Anawasilisha kazi yake ya muziki kwa lugha ya Kiingereza na lugha yake ya asili inayoitwa Twi. Mfalme huyu pia anaingia katika orodha ya wasanii kumi matajiri Afrika akiingiza mkwanja wa dola milioni 7 (zaidi ya bilioni 15 za Kitanzania).
Heshima yake ameijenga vipi?
Amejijengea heshima kwenye muziki wa Hip Hop hasa kutokana na kazi zake kuwa zenye ubora unaokubalika katika tasnia hiyo. Mpaka sasa amefanikiwa kutoa albamu nne zilizofanya vizuri kimauzo ambazo ni Makye (2009), Rapperholic (2012), Darkology (2014) na Mary aliyoiachia mapema mwaka huu.
Amewahi kuchukua mara kadhaa tuzo mbalimbali zenye heshima kubwa duniani kama vile (MTV na AFRIMA) katika vipengele vya Msanii Bora wa Hip Hop Afrika 2012 na 2013 na pia alikuwa msanii pekee wa Afrika kushirikishwa kwenye michano ya Black Entertainment Television (BET) maarufu kama Cypher mwaka 2012 pamoja na Talib Kweli, Jean Grae and Ab-Soul.
Ujasiriamali na uwekezaji
Miongoni mwa mambo yanayomfanya mfalme huyu kutengeneza mkwanja mrefu ni namna alivyojikita katika suala zima la ujasiriamali na uwekezaji akiwa na hisa kwenye Kampuni ya Tigo, Ghana.Anamiliki Studio inayoitwa Sarkcess Music, kituo cha kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, maduka ya nguo yanayofahamika sana nchini Ghana, Sark by Yas Clothing Line, ‘headphones’ zenye nembo ya Obidi na miradi mingine mingi.
New Guy yazidi kumng’arisha
Kwa sasa mfalme huyu anabamba na Ngoma ya New Guy aliomshirikisha Ice Wood kutoka Marekani.
Ikumbukwe pia hivi karibuni aliachia ‘dokyumentari’ iliyoangaliwa sana na mashabiki wa muziki duniani kote kwenye Mtandao wa Youtube inayoitwa New Guy inayozungumzia na kuonyesha harakati alizofanya mpaka kufanikisha kurekodi Wimbo wa New Guy na msanii mkubwa Marekani, Ice Wood.