Sarpong Aigomea Yanga

LICHA ya kusamehewa na kutakiwa kurejea kambini, lakini mshambuliaji wa Yanga, Mghana, Michael Sarpong ameonesha hali ya kugoma.

 

Hivi karibuni, Sarpong na Lamine Moro walirejeshwa kikosini baada ya nyota hao kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu.

Wakati Moro akiripoti kambini na juzi Jumapili kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, Sarpong hakuripoti.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, mshambuliaji huyo alitakiwa kuripoti kambini tangu Jumatano ya wiki iliyopita kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kumalizia msimu.

Mtoa taarifa huyo alisema sababu haijajulikana ya yeye kugomea kambi hiyo wakati timu hiyo ikijiandaa na fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Simba itakayopigwa Jumapili hii.

 

Sarpong bado hajarudi kazini, licha ya kusamehewa na kutakiwa kuripoti kambini tangu wiki iliyopita.

 

“Hivyo huenda asiwepo katika orodha ya wachezaji tutakaowatumia katika mchezo ujao wa Kariakoo Dabi dhidi ya Simba,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassani Bumbuli, kuzungumzia hilo, alisema: “Sarpong bado hajarudi kazini, licha ya kusamehewa, kuhusu kuachwa hilo mimi silifahamu.”

STORI: WILBERT MOLANDI, Dar


Toa comment