Sasa Wanalalamika Simba, Baadaye Itakuwa Yanga
LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea tena leo Ijumaa kwa mechi kadhaa ambazo zinatarajiwa kupigwa kwenye viwanja mbalimbali.
Ni ligi ambayo imeleta minong’ono mingi sana kupitia kwa mashabiki, wengi wameshaanza kuzungumza mambo mengi, wengine wakiamini kuwa kuna utaratibu mbovu sana kwenye ratiba ya ligi hiyo.
Baadhi ya watu akiwemo msemaji wa Simba, Haji Manara wameshaanza kutoa tahadhari juu ya kile ambacho kinatokea, hajasema moja kwa moja kuwa kuna kosa lakini ametumia mtandao wake wa kijamii kama vile kutoa tahadhari.
Ni kweli wengi wanaolalamika wapo sahihi kwa kuwa wanaona siyo sawa kwa timu moja kucheza michezo mingi nyumbani.
Yanga watacheza michezo 12 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, halafu baada ya hapo ndiyo watatoka nje ya Jiji la Dar es Salaam.
Tatizo hapa siyo Yanga, bali ni yale ambayo nilikuwa nasema siku zote kuwa kitendo cha kuwa na timu 20 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kina madhara yake.
Hii ni moja ya changamoto ya kuwa na timu 20 kwenye ligi, Yanga hawachezi Taifa michezo hiyo haina maana kwamba wanapendelewa bali wanacheza hapo kwa kuwa timu nyingi hazina uwanja wa kutumia.
Kwa sasa zaidi ya timu tano kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara zitakuwa zinatumia viwanja vyake Dar es Salaam na hivyo ni ligi ya ukanda mmoja.
Yanga, Simba, African Lyon, JKT Tanzania, Azam ni timu ambazo zipo Dar es Salaam na nyingi zinatumia Uwanja wa Uhuru, Chamazi na ule wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Haya ni matatizo kwa kuwa timu zote hizo hazina viwanja ndiyo maana inaonekana hali kama hiyo.
Kama African Lyon wangekuwa na uwanja wao Bagamoyo, Simba Chalinze na Yanga Mbande haya yote yasingetokea, lakini kwa kuwa TFF wanaruhusu hata uwanja ambao wanadang’anywa ndiyo wanatengeneza matatizo haya.
Shirikisho la Soka la Kimataifa ‘Fifa’ wakiuliza uwanja wa Simba upo wapi TFF wanawaonyesha Uwanja wa Taifa, wakiuliza Uwanja wa Yanga wanawaonyesha Taifa, Mtibwa Sugar, Taifa.
Nafikiri kama TFF wangekuwa makini kuhakikisha kuwa wanasimamia soka letu ipasavyo kila timu ingekuwa na uwanja.
Nimewahi kufuatilia kwa kipindi kifupi na kugundua kuwa TFF wanachangia kwa sehemu kubwa sana klabu zetu kutojenga viwanja kwa kuwa wanaonyesha kama siyo kitu muhimu kwenye soka.
Hii litakuwa tatizo kubwa kwetu kwa muda mrefu, na hali hii ndiyo inachangia soka letu linashindwa kukua kwa kasi inayotakiwa.
Kama TFF wakisimamia soka vizuri hakika haya yasingetokea, awali wakati wanaongeza timu kufikisha 20 wakati wa timu 16 bado nusu ya timu zilikuwa zimejikusanya kwenye kanda moja jambo ambalo pia lilisababisha mechi nyingi kuchezwa sehemu ndogo.
Swali kubwa la kujiuliza ni kwamba mwishoni mwa msimu huu Yanga nao watalalamika kuwa Simba amemalizia mechi nyingi nyumbani kwa kuwa kama Yanga wanacheza hapo sasa lakini ifahamike kuwa Simba nao watacheza hapo na idadi ya michezo inafanana.
Kwa sasa inazungumzwa ya Yanga kwa kuwa ndiyo ipo kwenye mzunguko wa kwanza lakini baadaye itazungumzwa ya Simba kwa kuwa nayo lazima itachezwa kwenye ligi hii.
Na haya yatakuwa malalamiko ya klabu na TFF kwa kila msimu hadi pale timu zitakapokuwa na viwanja vyao ambavyo zitakuwa zikivitumia.
Ni Mtazamo Wangu – PHILLIP NKINI
Comments are closed.