Sawa Jamani..! Lakini Usimwambie ! – 10
Irene Mwamfupe Ndauka
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Moreen akampigia simu Alfa…
“Baby ndiyo nimefika nje hapa…”
“Ingia namba kumi na mbili…”
SASA ENDELEA MWENYEWE…
“
Oke, ndiyo naingia ndani sasa,” alisema Moreen kwa sauti ndogo huku akipita vyumba mbalimbali kuanzia namba mbili hadi alipofika mlango wa chumba namba kumi na mbili, akasimama hapo kisha akatikisa kitasa cha mlango wa chumba hicho na kusubiri kufunguliwa.
Ina maana kwamba, aliposimama Moreen alibakiza hatua moja tu kifikia mlango wa chumba namba kumi na tatu ambacho mumewe na mke wa Alfa walikuwemo ndani wakipasha…pasha!
***
Kule chumbani, Kizito na mke wa Alfa walikuwa wakiongea kama wako nje lakini wakijiamini kuwa, wapo salama salimini…
“Kizito mpenzi, unajua nini? Nilikupendaga tangu zamani sana, ila basi tu. Unajua mke wa mtu ni mke wa mtu. Sijui nini kilikufanya ujitokeze leo kwenye simu tena kwa kuniambia kitu ambacho si cha kweli, labda ni mungu mwenyewe,” alisema mke wa Alfa…
“Ni kweli kabisa, mimi mwenyewe pia nilijiuliza inakuaje nikupigie simu kwa jambo nililoongea na mzee na tukamalizana,” alisema Kizito. Hapo mkono mmoja ulikuwa kwenye mwili wa mwanamke huyo ukitalii mpaka basi.
Ilifika mahali, mke wa Alfa aliweweseka sasa kwani uchokozi wa Kizito ulimzidi. Kila alipoamini kuwa, sasa Kizito amefika mwisho, ataingia hatua nyingine ya kuanza mechi, yeye alizidi kubaki palepale tu na kumzidishia muwashawasha mwanamke huyo.
***
“Mh! Kuna watu wanafanana sauti jamani! Huyo mwanaume anayeongea huko chumba cha pili utasema mume wangu Kizito.”
Hapo, Moreen alishaingia chumbani na kupokelewa na Alfa kwa mabusu motomoto, lakini kuhusu sauti hiyo aliamua kutoa dukuduku lake kwa Alfa…
“Yaani baby hiyo sauti naisikia mlango wa pili huko, mume wangu mume wangu kabisa…”
“Ah! Kweli? Au kaja na mchepuko wake?” alisema Alfa na kucheka kama vile ni utani tu…
“Aje naye tu, mimi sijali, ilimradi nisijue na anichungie heshima yangu,” alisema Moreen kwa sauti yenye wivu licha ya kujipa ujasiri.
Alfa akacheka sana kisha akanyamaza, wakazama mahabani kwa kaunza na denda.
***
Kule chumbani kwa akina Kizito, mke wa Alfa hakuwa akipenda feni wala madirisha kufungwa, hivyo akayafungua ili upepo wa asili uingie ndani.
Kitendo hicho kilisindikiza sauti kusikika zaidi kutoka kwenye chumba hicho, hasa sauti ya Kizito mwenyewe.
Moreen alijikuta akikaza macho kusikiliza. Kwa asilimia themanini na tano aliamini ni mume wake lakini kumi na tano zilizobaki alisema siye kwa sababu alimwambia yupo ofisini. Lakini akaamua kumtumia meseji…
“Sweet umesema upo job au wapi?”
Meseji hiyo ilipokwenda, upande wa chumba hicho kukawa na ukimya kitendo ambacho, Moreen alikitafsiri kama mumewe sasa alikuwa akiisoma meseji yake.
Baada ya muda, meseji ilirudisha majibu…
“Yes baby karibu sana kama wataka kuja,” alijibu Kizito akijua kwamba mkewe mpaka ajiandae, atoke, yeye atakuwa amesharudi ofisini kwake…
Alfa alishangaa hali ya Moreen kuwa bize na simu…
“Moreen unataka kunikamatisha nini? Mbona upo kwenye simu sana? Si ajabu unawasiliana na mista, unampa ramani ya hoteli tulipo…”
“Mmm! Jamani si kweli…kuna mtu hapa namtumia meseji ndiyo maana…”
“Unamtumia meseji nani?”
“Dada yangu mmoja hivi, aliniuliza kama nipo nyumbani,” alisema Moreen akidanganya.
Kutoka moyoni mwake hakupenda kusema ukweli kuhusu alichoendelea kukisikia kutoka kwenye chumba hicho kwamba, mwanaume aliyekuwemo anakaribia kwa asilimia kubwa kuwa mume wake.
Moreen akaiweka simu kwenye stuli, akapanda kitandani na kuanza kucheza na Alfa lakini akili ilikuwa haipo sana pale.
***
Kizito na mke wa Alfa waliingia hatua ya pili ya mbwembwe kwani sasa waliingia uwanjani na mpira ulikuwa ukipigwa kwelikweli, mashambulizi yakianza huku, hayasimami mpaka yafike upande wa pili.
Mke wa Alfa akafika kwenye uhalisia wake ambapo huweweseka kwa maneno mengi na sauti ya kusikika chumba cha pili.
Hali hiyo ilimfikia Alfa kule chumbani, naye akashtuka kwani mke wake anamjua, kelele zake anazijua na vikorombwezo vingine vyote anavijua…
“Mh! Aliguna Alfa hasa pale, mkewe alipokuwa akisemasema maneno kama anatangaza mpira wa watani wa jadi…
“Mbona umeguna baby, hao watu wanakupa joto na wewe nini?” aliuliza Moreen, akaendelea…
“Ndiyo tabia ya watu wa uswahilini siku wakifika maeneo kama haya, kelele nyingi, kama ni wao tu. Sasa hao uwafaidi kwenye nyumba za kupanga, wee! Mbona mtazima redio muwasikilize wao tu.”
Wakati, Moreen akisema hayo, mwenzake alikuwa mbali kimawazo. Kelele za upande wa pili zilimtibua sana…
“Huyo ni mke wangu kabisaa mama naniii, maana ndiye mpiga kelele hizo,” alisema moyoni Alfa.
Moreen alijitahidi sana kumrejesha Alfa kwenye mawazo ya pale kitandani lakini wapi…
“Baby, mbona leo si kama siku ile halafu ghafla tu, kuna nini?” aliuliza Moreen, Alfa akajipa ujasiri wa kutosema lakini akaanza kuwaza…
“Huyu alisema anasikia sauti kama ya mume wake, mimi nasikia sauti kama ya mke wangu. Inakuaje haya mambo?”
Moreen alifika mahali akaamua kushuka mpaka ngazi ya kati akiamini pengine atamuweka sawasawa mpenzi wake huyo lakini wapi! Alitumia mpaka maneno, kusema sana na kuimba juu, lakini Alfa wala! Akawa mbaali!
Kelele zaidi kutoka kwenye chumba cha pili zilizidi kumpa wakati mgumu Alfa, lakini kwa Moreen zilimfanya azidishe manjonjo lakini wapi! Alfa, akaamua kufunguka sasa…
“Moreen, hakyanani huyo mwanamke anayepiga kelele huko chumbani ni mama Shaban…”
“Mama Shaban ndiye nani sweet?”
“Mke wangu…”
“He! Yaani mimi niwe na wasiwasi na mume wangu halafu wewe uwe na wasiwasi na mkeo, acha utani darling, unajua ni hatari sana kuwaza hivi,” alisema Moreen…
“Moreen nakuapia, huyo ni mama Shebby, ni yeye kwa asilimia mia moja na hamsini, mimi namjua bwana,” alijiapiza Alfa na kuzidi kunyong’onyea kila idara…
“Sasa tunafanyaje dear? Mbona kama ni tatizo kubwa” alisema Moreen akiinuka na kukaa kitandani…
Je, unajua nini kilitokea? Usikose kusoma wiki ijayo.