SBL kuendelea kuchangia maendeleo ya kilimo nchini kupitia elimu

Kampuni ya Bia ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imedhamiria kuendelea kutengeneza maisha bora kwa vijana na wakulima nchini kupitia programu yake ya udhamini wa masomo kwa wanafunzi wanaotoka familia masikini kwenye vyuo vinavyofundisha kilimo.
Programu hii iliyoanzishwa mwaka 2010 imesaidia wanafunzi 71 kusomea kozi za diploma katika ujuzi wa kilimo katika vyuo vinne kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa SBL, Mark Ocitti.
Katika tukio la kuwapongeza wanafunzi 17 waliopata nafasi za ufadhili kupitia programu hii kutoka chuo cha Mt Maria Goretti Agriculture Training Institute, Ocitti alinukuliwa akisema kuwa Kilimo Viwanda imelenga kusaidia wanafunzi kutoka familia masikini ili waweze kusomea masomo ya kilimo kwenye ngazi ya diploma katika vyuo vya ndani.

Wanafunzi wengine 43 chini ya programu hii wanapatikana Kaole Wazazi College of Agriculture (Bagamoyo), Kilacha Agriculture and Livestock Training Institute (Moshi) na Igabiro Training Insitute of Agriculture (Bukoba).
Ocitti alifafanua kuwa ufadhili huu unajumuisha malipo yote ya chuo na gharama zingine katika kipindi chao chote cha masomo. Vilevile, Kilimo Viwanda inalenga kuongeza nguvu
jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuongeza idadi ya wataalamu wa mashamba watakaowasaidia wakulima kuboresha mashamba yao. SBL inategemea kwa kiasi kikubwa mazao ya nafaka kama vile mtama, shayiri na mahindi katika uzalishaji wao.
Vile vile Ocitti alisema, ‘Programu hii ni fursa nzuri kwa wanafunzi kuongeza upeo wao kwa kujifunza kimatendo watakapotembelea mashamba makubwa ya wakulima wanaolima nafaka kama hizi pamoja na kutembelea viwanda vyetu vya Dar es Salaam, Moshi na Mwanza ili kushuhudia namna kilimo na uzalishaji unavyotegemeana.’

Mkuu wa Chuo hicho, Isaya Marcus Kigava hakuwa nyuma kusema, ‘naipongeza na kuishukuru sana kampuni ya Serengeti kwa kusudi lao zuri la kuwasaidia wanafunzi hawa katika kuboresha maisha yao ya baadae. Ni programu muhimu sana kuwapa elimu ya kimatendo ili waweze kufanya vyema kwenye kilimo cha biashara. Daima tutaukumbuka mchango wenu’
SBL inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka vyuo vinne kwenye programu hii ya Kilimo Viwanda ambavyo ni; Kaole Wazazi College of Agriculture (Bagamoyo) ambapo wanafunzi 15 tayari washatangazwa; Kilacha Agriculture and Livestock Training Institute (Moshi), na Igabiro Training Insitute of Agriculture (Bukoba) watakaotangazwa siku za usoni.
Stori: Na Mwandishi Wetu

