The House of Favourite Newspapers

Sekondari St. Matthew Yafunguka Kuzuiliwa Matokeo na Baraza la Mitiani

 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitiani, Dk Charles Msonde.

 

Uongozi wa shule ya sekondari St. Matthew unatoa pole kwa vijana wetu 228 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2018 ambao matokeo ya jitihada, nguvu, jasho na kujikana kwao kwa miaka 4 yamezuiliwa kutoka mpaka sasa kwa kilichoelezwa kusubiri uchunguzi wa tuhuma za udanganyifu katika mitihani yao ya taifa. Tunawapa pole wazazi, walezi, walimu, ndugu, jamaa na marafiki pia kutokana na maumivu na taharuki wanayopata kutokana na kuchelewa kutoka kwa matokeo ya watoto wao na namna wanavyoona vijana wetu wanaumia na kutaabika sana.

 

Baada ya kusubiri kwa muda mrefu, tangu tarehe 24/01/2019 matokeo yalipozuiliwa tukitegemea kupata ufafanuzi wa kina kutoka mamlaka husika, tumeona hatuwezi kuendelea kukaa kimya bila kuwajulisha vijana wetu na watanzania tunachofahamu kama shule na hatua ambazo tumeshachukua.

 

Kwanza kabisa tungependa kuufahamisha umma, kama shule taarifa ya kuzuiliwa kwa matokeo ya vijana wetu tumezipata kupitia vyombo vya habari kama ambavyo ilielezwa wakati wa kutangaza matokeo. Tulichukua hatua mara moja kwa kuandika barua Baraza la Mitiani siku hiyo hiyo kuuliza kuna sababu gani ya kuzuiliwa kwa matokeo ya vijana wetu, lakini mpaka sasa hatujapokea taarifa yoyote kutoka mamlaka yoyote, iwe ya elimu au ya kiuchunguzi, kuhusiana na kasoro au tuhuma zozote za udanganyifu kwenye mitihani iliyomalizika ya kidato cha nne mwaka 2018.

 

Hivyo basi, hata sisi kama shule hatufahamu hizo tuhuma za udanganyifu anatuhumiwa nani na zilifanyika wakati gani. Tunachofahamu ni kwamba kwa kipindi chote kabla ya mitihani, wakati wa mitihani na baada ya mitihani, taratibu na kanuni za Baraza la Mitiani zilifuatwa na hakuna kasoro yoyote iliyojitokeza au kuripotiwa kwetu na mamlaka zilizosimamia mitiani hiyo, zaidi tu tulipongezwa kutokana na nidhamu kubwa waliyoonyesha vijana wetu kipindi chote cha mitihani na walimaliza na kuondoka kwa furaha na amani.

 

Lakini pia tungependa kuufamisha umma kuwa, kwa mujibu wa muongozo wa taratibu za mitihani ya taifa, shule baada ya kukidhi vigezo husajiliwa kama kituo cha mitiani tu na haihusiki na mitihani hiyo zaidi ya kutoa vyumba vya kufanyia mitihani na watahiniwa waliosajiliwa, lakini taratibu nyingine zote kuanzia kupokea mitihani, kusimamia watahiniwa na vyumba vya kufanyia mitihani, kukusanya na kufunga mitihani na mambo mengine yote yanayohusiana na mitihani, hufanywa na Baraza la Mitiani kupitia maafisa wake wanaokuwa

 

wamepangwa katika kituo cha mitihani. Na kwa upande wa shule yetu, mitiani huwa hailali shuleni, yote huletwa siku ya mitihani husika na kuondoka inapokamilika siku hiyo hiyo.

 

Hivyo basi, uongozi unapenda kuwatoa hofu vijana wetu, wazazi, walezi, wadau wetu kwenye elimu, ndugu, jamaa na marafiki kwamba, kwakuwa kama shule hatujatuhumiwa wala kuhusishwa kwa namna yoyote kwenye uchunguzi au tuhuma hizi, ni wazi kwamba shule yetu HAIHUSIKI KWA NAMNA YOYOTE ILE na tuhuma hizo. Sisi kama ilivyo kawaida yetu tutaendelea kuwahudumia vijana wa Tanzania kwa kuwafundisha nidhamu, maadili mema na kuwapatia elimu iliyo bora sana na kuwaandaa vizuri ili kukabiliana na ushindani wa kitaaluma na kimaadili popote watakapokwenda ndani na nje ya nchi. Ndani ya miaka miwili hii tumefanya mabadiliko makubwa katika mfumo wetu na namna ambavyo tunawalea na kuwafundisha vijana wetu, lengo likiwa kuendelea kutoa huduma ya kuelimisha vijana wetu kwa kuwapa kipaumbele vijana ambao hawakuchaguliwa kujiunga na shule za serikali au kuachwa kwa kigezo cha ufaulu, na kuwafudisha kuwa bora zaidi ili jamii ielewe kwamba vijana wetu wote wana uwezo wa kufundishwa na kufanya vizuri katika masomo yao bila kujali huko nyuma alifaulu kwa kiwango gani na msisitizo wetu ukiwa kwenye NIDHAMU.

 

Ni rai yetu kwa Baraza la Mitiani na mamlaka zote zinazohusika kulipatia ufumbuzi swala la kuachiwa kwa matokeo ya vijana wetu mapema inavyowezekana ili vijana wetu wasiendelee kuteseka. Sisi kama shule hatuna mashaka kabisa na utendaji wa serikali kwa sasa, tunaamini mamlaka zina wajibu wa kuzifanyia kazi kasoro zozote zinazojitokeza katika mitihani ili kuhakikisha hazijirudii tena na kuongeza thamani na umuhimu wa mitihani ya taifa katika kuzalisha vijana wenye uelewa mpana na wa kiushindani.

 

Mwisho, tunawaomba vijana wetu ambao matokeo yao yamezuiliwa, wazazi, walezi, ndugu, jamaa na marafiki, kuwa watulivu katika kipindi hiki na kuzipatia mamlaka zinazohusika nafasi ya kufanya kazi zao, tunaamini muda si mrefu matokeo ya vijana wetu yataachiwa, kwakuwa kama shule tunahakika tuliwaandaa vizuri vijana wetu na wamefaulu mitiani yao kwa kiwango kikubwa bila udanganyifu wowote.

SISI NI NIDHAMU, KUFAULU NI UTAMADUNI WETU.

Mkuu wa Shule

12/02/2019

Comments are closed.