The House of Favourite Newspapers

Selena Gomez Amwaga Machozi Kisa Sera za Trump Kufukuza Wahamiaji Haramu

Mwanamuziki na muigizaji maarufu duniani, Selena Gomez amejirekodi akiwa anamwaga machozi kwenye Instastori yake alipokuwa akizungumzia sera ya Rais Donald Trump ya kuwaondoa wahamiaji haramu wa Mexico kutoka Marekani na kuwarudisha makwao.

Kupitia Instagram account yake yenye zaidi ya followers milioni 400, Selena mwenye umri wa miaka 32 alilia kwa uchungu huku akijibu tishio la Rais Trump la kuwafukuza wahamiaji wote wasiokuwa na vibali, jambo ambalo limeibua hofu kubwa ya familia nyingi kutenganishwa.

“Watu wangu wote wanashambuliwa, watoto. Sielewi. Nasikitika sana, natamani ningefanya kitu lakini siwezi. Sijui nifanye nini. Nitajaribu kila kitu, naahidi,” alisema katika video hiyo ambayo ilifutwa muda mfupi baadaye.

Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE), Jumapili iliyopita msako wa kitaifa dhidi ya wahamiaji haramu ulisababisha kukamatwa kwa watu 956, idadi kubwa zaidi tangu Trump alipochukua tena madaraka.

Selena Gomez amekuwa mtetezi wa wahamiaji, hususan wale wanaotoka Mexico, kwani baba yake mzazi ana asili ya Mexico, huku mama yake akiwa na asili ya Italia.