The House of Favourite Newspapers

SERIKALI CHINA YAPIGA MARUFUKU HARUSI ZA KIFAHARI

SERIKALI ya China ipo mbioni kudhibiti ongezeko la harusi za kifahari ambazo zimekuwa zikishamiri katika miaka ya karibuni. 

 

Kwa mujibu wa maofisa wa serikali, harusi za kisasa si tu ni za gharama kubwa bali zinaenda kinyume na misingi ya kijamaa ya nchi hiyo. Harusi za Kichina ambazo hufungwa kimila, huambatana na sherehe ambazo kwa sasa serikali inadai zimekuwa za gharama kubwa mno. Hivi sasa serikali inajipanga kuja na namna ya kuzifanya ziwe za kiasi cha kawaida.

 

Wachina kama ilivyo kwa raia wa nchi nyingine duniani wamekuwa wakishindana na majirani, marafiki na jamaa katika kuandaa sherehe kubwa na za kupendeza za harusi, jambo ambalo limekuwa ni fasheni sasa. Harusi hizo huambatana na karamu kubwa, nguo za kifahari na safari za ughaibuni ili kupiga picha za harusi. Wageni pia hutarajiwa kupeleka zawadi za kifahari. Pia, utaratibu wa asili wa kuwafanyia stihizai (mzaha) bibi na bwana harusi kabla ya ndoa – ili kuwaondolea woga katika siku yao kubwa- pia umetajwa kufanyika katika namna isiyokubalika katika siku za hivi karibuni.

 

Kumekuwa na ripoti kuwa wahudhuriaji harusi wamekuwa wakiwafanyia wanandoa vitendo vya stihizai vinavyodhalilisha na wakati mwengine hugeuka shambulio. Wiki iliyopita bwana harusi mmoja aligongwa na gari wakati akikimbia utaratibu huo ambao alikuwa afungwe kamba na kupigwa. Wiki mbili zilizopita, wapambe wa bibi harusi mmoja walijeruhiwa na vipande vya vioo baada ya wapambe wa bwana harusi kulazimisha kuingia katika nyumba yao kwa kuvunja mlango na shoka.

 

Wizara ya mambo ya kijamii ya nchi hiyo imelaani vikali matukio hayo “ya kifahari na upuuzi” na kutoa “mwongozo” wa kufanya harusi “ndogo na za sherehe za kiasi”, shirika la habari la Xinhua limeripoti. “Sherehe zinapaswa kuzingatia misingi ya kijamaa na tamaduni za China ili kudhibiti mienendo hasi na kuwa mfano kwa jamii nzima. Mamlaka zitatunga kanuni za mchakato wa harusi na ukomo wa zawadi na fedha,” ofisa wa wizara hiyo, Yang Zongtao, aliiambia runinga ya serikali Jumapili.

 

Hii si mara ya kwanza kwa China kujaribu kuwaelekeza wananchi wake namna ya kusherehekea ndoa zao.Mwaka 2016, Chama cha Kikomunisti kinachoongoza nchi hiyo kilitoa rasimu ya mwongozo wa kusherehekea harusi kwa kuzingatia misingi ya chama hicho ya kubana matumizi yasiyo ya lazima.

 

Comments are closed.