The House of Favourite Newspapers

Serikali Isaidie Katika Hili la Kupaa Kwa Bei ya Vyakula

0

Na Eric Shigongo, Uwazi, Napasua Jipu

NIMSHUKURU Mungu kwa kunipa uhai na afya tele leo lakini pia kwa kuwaweka hai nyinyi wasomaji wa makala haya, hakika wote tumhimidi yeye. Wiki iliyopita tulimsikia Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alipokuwa akisoma bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/ 18 akisema kwamba bei ya mazao ya vyakula imepanda kwa asilimia 56. Ni kiwango kikubwa sana. Mfano wa wazi ni bei ya unga wa mahindi, umepanda mno sokoni na zao hilo ni kimbilio la wanyonge. Wengi wanaoshindwa kula ugali kutokana na kuwa na unga kidogo, huamua kupika uji na watu wakanywa na kulala kusubiri kesho. Unga wa mahindi unapofikia shilingi 2,200 kwa kilo moja ni tatizo kubwa sana. Kunakuwa hakuna tofauti kati ya unga wa mahindi na mchele. Unga wa mahindi umekuwa ghali sehemu nyingine kuliko hata petroli! Ni hatari.

Miaka ya nyuma tulishuhudia mchele ukionekana ni chakula cha hadhi kiasi kwamba baadhi ya familia walikuwa wakipika wali siku maalum tu kutokana na ukweli kwamba bei yake ilikuwa juu lakini leo unga wa mahindi umepiku mchele na haishikiki. Inashangaza. Mwishoni mwa Aprili waandishi wetu walifanya uchunguzi mdogo na kubaini kuwa bei ya unga ilikuwa kubwa kuliko mchele, lakini pia bei ya maharage ambayo nayo miaka ya nyuma ilikuwa ni nafuu sana, sasa inakaribia bei ya kilo moja ya nyama. Katika uchunguzi huo tulibaini kwamba bei ya kilo moja ya unga ni shilingi 2,200 hadi shilingi 2,500 na bei ya mchele ni kati ya shilingi 1,500 hadi shilingi 2,200 na maharage ni shilingi 2,200 kwa kilo.

Ukweli ni kwamba bei hizo hazileti matumaini mema kwa wananchi wa kawaida ambao miaka nenda rudi chakula chao kikuu ni ugali wa mahindi na maharage. Ndugu zangu, kutokana na hali hiyo basi ni vema kwa serikali kuangalia jinsi ya kuhakikisha bei ya bidhaa hizo zinapungua badala ya kungoja mpaka Julai kama alivyosema Naibu Waziri wa Kilimo, Mifungo na Uvuvi, William Ole Nasha. Ole Nasha alisema kupanda kwa unga kulitokana na uhaba wa nafaka za mahindi na hata maharage mwaka 2016. Alisema hali hiyo haitarajiwi mwaka huu kwa kuwa mahindi mengi yanatarajiwa kuvunwa.

Je, hakuna njia nyingine ya kufanya bali tutegemee kauli ya naibu waziri aliye na matumaini kwamba mwaka huu mahindi yatavunwa zaidi? Hakuna njia mbadala kama vile serikali kununua mahindi kisha kuwagawia wasagishaji wakubwa ili wauze kwa bei nafuu kwa wauzaji wa unga wa mitaani? Watu wanaumia jamani! Nashauri, ipo haja ya kuhakikisha taifa linajipanga katika tatizo hili ili kupunguza makali yanayowakabili wananchi walio wengi, hasa wa kada ya chini ambako ndiko hasa bei hizi za juu zinawaumiza kwa kushindwa kujikimu. Naungana na wabunge na wasomi walioshauri kwamba, wakati tunasubiri mavuno makubwa ya mwaka huu yanayotarajiwa kuvunwa na wakulima wetu, kwa sasa serikali haina budi kuingilia kati mfumuko huu wa bei ili wananchi waishi kwa furaha na amani.

Njia nyingine ambayo serikali inaweza kufanya ni kutoa akiba ya chakula kwenye maghala yake na kuingiza sokoni kwa nia njema ya kuhakikisha mfumuko huu wa bei ya vyakula hasa unga wa mahindi, unadhibitiwa. Nasema hivyo kwa sababu lazima tujifunze kwamba kwa miaka hii ya leo ambapo tabia nchi imebadilika, tabia ya kutegemea mvua kwenye kilimo, haiaminiki tena na kwa dunia ya sasa hayo ni mambo yaliyopitwa na wakati.

Ukweli ni kwamba kama tumedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa kati, ni lazima kama taifa tuwe na chakula cha kutosha na kipatikane kwa bei nafuu ambayo itafanya kila mwananchi amudu. Lakini kwa miaka ijayo, serikali lazima ihakikishe tunaondokana na kilimo cha kutegemea mvua kwani kwa kutegemea mvua, hatuwezi kuwa na chakula cha kututosheleza. Ushauri wangu kwa serikali na wadau wa kilimo, wakati umefika wa kuhakikisha tunalima chakula kingi kwa njia ya umwagiliaji na kuachana na kutegemea mvua kwani nchi yetu ina vyanzo vingi vya maji yanayoweza kutumika kwa kilimo sehemu mbalimbali. Uzuri ni kwamba nchi yetu ina rutuba yakutosha. Bila kufanya hayo, wananchi wataendelea kupata machungu na kamwe hatuwezi kuwa nchi iliyopiga hatua kiuchumi. Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply