The House of Favourite Newspapers

Serikali Kuongeza Umri, Sifa Ya Kupata Mikopo Ya Asilimia 10 Ya Halmashauri

Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange

Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Serikali imeongeza umri wa ukomo katika mikopo ya asilimia 10 itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vijana kutoka miaka 35 hadi 45 ili kuweza kufikia vijana wengi zaidi.

Mhe. Dkt Dugange ameyasema hayo wakati wa akijibu swali Mhe. Venant Daud Protas Mbunge wa Jimbo la Igalula katika kipindi cha maswali na majibu aliyeuliza “Je, Serikali haioni haja ya kuongeza umri kwa Vijana wa kiume wanaopata mikopo ya Halmashauri kufikia miaka 50.” katika Bunge la bajeti linaloendelea Jijini Dodoma.

Amesema, Mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kifungu cha 37A ya Mwaka 2018 na Kanuni za Usimamizi na Utoaji wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za Mwaka 2024.

”Kwa mujibu wa Sheria hii, mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo isiyo na riba. Makundi haya yana fursa ndogo ya kupata mikopo katika taasisi nyingine za fedha kwa kuwa yanakosa dhamana na uwezo mdogo wa kumudu riba. Aidha, umri wa ukomo katika mikopo kwa vijana umeongezwa kutoka miaka 35 hadi 45.” amesisitiza

Amesema pia, Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa mikopo hii kwa mujibu wa sheria na kanuni, na kufanya maboresho pale itakapohitajika ili kuhakikisha ufanisi na uwiano katika utoaji wa fursa hizi.