Serikali Kushirikiana na Vyombo vya Habari, Kutangaza Malengo na Mikakati ya SADC

Ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wanahabari mjini Bagamoyo mkoani Pwani

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa, itaendelea kushirikiana na makundi mbalimbali katika jamii vikiwemo vyombo vya habari ili kuhakikisha wanayafahamu malengo na mikakati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waweze kuibua fursa mbalimbali zilizopo katika nchi wanachama kwa lengo la kuwashirikisha Watanzania waweze kuzitumia kujiendeleza.

 

Hayo yamesemwa leo Julai 25, 2022 na Balozi Agnes Kayola wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine katika ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wanahabari mjini Bagamoyo mkoani Pwani yanayoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

 

Lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uelewa wanahabari kuhusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili waweze kushiriki kikamilifu kutoa taarifa chanya ambazo zitakuwa na hamasa kwa Watanzania waweze kuzitambua fursa zilizopo katika jumuiya hiyo.

Balozi Agnes Kayola

“Tanzania ni miongoni mwa nchi waanzishi wa SADC ambayo ina umri wa miaka 40. Waandishi wa habari mna mchango mkubwa kuhakikisha kundi la vijana linafahamu ipasavyo umuhimu wa SADC ili waweze kushiriki na kuzitumia fursa zilizopo katika jumuiya hii ya kikanda kwa manufaa,”amesema Balozi Kayola.

 

Amesema, licha ya fursa nyingi zilizopo katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo, pia Tanzania inazo huduma nyingi ambazo zikitumika ipasavyo zitaweza kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

 

“Pia kutokana na fursa zinazopatikana tutaendelea kutumia lugha yetu ya Kiswahili kama bidhaa, hivyo jukumu kubwa ambalo mnapaswa kulifahamu ni kuhakikisha mnakitumia Kiswahili ipasavyo katika kutoa taarifa zenu,”amesema.

Malengo ya mafunzo hayo ni kutangaza malengo na mikakati ya SADC

Amefafanua kuwa, malengo ya SADC kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha 5 cha Mkataba wa SADC (1992) ni kufikia maendeleo ya kiuchumi, amani na usalama, na ukuaji, kupunguza umaskini, kuimarisha kiwango na ubora wa maisha ya watu wa Kusini mwa Afrika.

 

Sambamba na kusaidia watu wasiojiweza kijamii kupitia Ushirikiano wa Kikanda. “Malengo haya yanapaswa kufikiwa kwa kuongezeka kwa Mtangamano wa Kikanda, unaojengwa kwa misingi ya kidemokrasia, na maendeleo yenye usawa na endelevu,”amesema.

4231
SWALI LA LEO
YANGA/SIMBA KIMATAIFA
Baada ya usajili wa nguvu, mechi za Siku ya Wananchi na Simba Day kisha mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Ngao ya Hisani, je, ni timu gani unaamini itafanya vizuri kimataifa?Toa comment