The House of Favourite Newspapers

Serikali Kuzingatia Maendeleo ya Viwanda Dira ya 2050

· CTI nayo yaweka mkazo wakikutana Dar

0

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema katika maandalizi ya dira ya taifa  2050 imeweka kipaumbele kikubwa kwenye maendeleo ya ya viwanda ili kuondoa utegemezi wa kununua bidhaa nyingi nje ya nchi.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, wakati akizungumza kwenye mkutano wadau wa viwanda.

Mkutano huo ulioandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), pia ulizindua tuzo za Rais za Mzalishaji Bora Viwandani PMAYA ambazo hufanyika kila mwaka kwa wenye viwanda.

Profesa Mkumbo alisema wasomi mbalimbali wamesema kwenye maandiko yao kuwa tofauti kubwa baina ya nchi tajiri na zile maskini ni kwamba nchi tajiri zina viwanda vingi wakati nchi maskini hazina viwanda na zinategemea kununua bidhaa nje ya nchi.

“Itakuwa vigumu sana kutengeneza dira ya taifa bila kuweka viwanda katikati ya dira hiyo kwasababu hilo ni la msingi na hatuwezi kuendelea bila kuwa na viwanda vingi,” alisema

Alisema katika utafiti ambao umefanywa na serikali katika maandalizi ya dira hiyo uliohusisha watu 7,668 nchi nzima waliochaguliwa kisayansi walitaka vipaumbele vitano viwepo kwenye dira hiyo.

Alitaja moja ya kipaumbele kilichotajwa na wananchi hao kuwa ni suala la viwanda na kwamba asilimia 65 ya malighafi zinazotumika viwandani zinatokana na kilimo  hivyo kilimo nacho kitaendelea kuwa kipaumbele kwenye dira hiyo.

Alisema kipaumbele kingine kilichotajwa kwenye utafiti huo ni uwekezaji mkubwa kwenye rasilimali watu kwani uchumi wa viwanda unahitaji watu waliosoma vizuri.

“Lazima dira yetu ituelekeze kuwekeza kwenye elimu na siyo elimu tu bali elimu iliyobora,” alisema Profesa Mkumbo.

Naye Mwenyekiti wa CTI, Leodegar Tenga alisema wadau wa viwanda wamekutana kujadili dira ya 2050 na kuzungumzia maendeleo ya viwanda kwa ujumla ili kuhakikisha maendeleo ya viwanda hayasahauliki kwenye dira hiyo.

“Tunashukuru Waziri amezungumza kwamba bila viwanda hakuna maendeleo na ametoa mifano ya nchi nyingi zilizoendelea namna zilivyopiga hatua kwenye viwanda,” alisema Tenga

“Hakuna nchi duniani hata moja ambayo iliwahi kupiga hatua kubwa kiuchumi bila kuwekeza kwenye viwanda kwa hiyo lazima tuwe na mikakati madhubutu na kuna msemo wa Kiswahili kwamba kupanga ni kuchagua kwa hiyo tuchague kuwekeza kwenye viwanda ili tusonge mbele,” alisema

Alisema ili viwanda viweze kufanyakazi vizuri lazima serikali iwekeze pia kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli na kuwekeza kwenye rasilimali watu.

“Maono ya nchi ni kujipanga ili tutimize tulichopanga kwa hiyo sisi CTI tunaamini viwanda ni muhimu na ili kupata rasilimali lazima tuwe na kilimo kwa hiyo lazima tuwekeze pia kwenye kilimo,” alisema

“Tumefungua masoko mengi upande wa Afrika Mashariki (EAC),  kusini mwa jangwa la sahara (SADC) sasa tujipange kuuza bidhaa zetu za viwandda nje ya nchi badala ya sisi kuwa soko la bidhaa za wenzetu,” alisema Tenga

Makamu Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza alisema nchi inapaswa kuwa na viwezeshaji vinavyofaa kama teknolojia, rasilimali watu na miundombinu.

“Zaidi ya hayo, ni lazima tujenge msingi imara wa amani, utulivu, umoja, kujitegemea, na muundo wa utawala unaounga mkono uwajibikaji, uwazi na kufanya maamuzi shirikishi,” alisema.

“Lazima tutafakari kuhusu maisha yetu ya zamani, tuelewe maisha yetu ya sasa, na kwa ujasiri kuunda maisha yetu ya baadaye na tunahitaji maono wazi yanayoungwa mkono na chaguzi za kimkakati na inayoungwa mkono na maadili,” alisema.

Leave A Reply